Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Baba jana, kumekuwa na mwamko mdogo wa watu kusherehekea sikukuu hiyo tofauti na ya Mama.
Jana, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), lilitoa taarifa yake na kuwakumbusha wazazi wa kiume namna wanavyopaswa kuzingatia malezi ya watoto wao hasa wakati wakiwa katika umri mdogo.
Siku ya Baba Duniani huadhimishwa kila ifikapo Juni 17.
Unicef ilisema mzazi wa kiume anayejitahidi kuwa karibu na mtoto tangu akiwa katika umri mdogo, ana nafasi kubwa ya kuwa kichocheo cha maendeleo ya watoto.
Unicef imesema tafiti zinaonyesha pia watoto wanapokuwa na ukaribu wa kipekee na wazazi wao wa kiume wapo kwenye mwelekeo mzuri wa kuwa na afya njema kisaikolojia, kujiamini na kutosheka katika mfumo wa maisha.
Hata hivyo, wanaume wengi waliohojiwa na Mwananchi wamesema tamaduni na mila za Kiafrika ndizo zimesababisha siku hii isipewe kipaumbele hasa kwa nchi za Afrika.
“Huku kwetu haya mambo hatuyapi kipaumbele sana kwa sababu nyingi ikiwamo zile zilizosababishwa na historia ya makuzi yetu. Haya mambo hatujawahi kuwa nayo hapo kabla....yameingia katika siku za hivi karibuni hivyo ni vigumu kuwakuta kina baba wakiyachangamkia,” alisema Walter Tosha baba wa watoto wa wawili na mmoja wa wanaume waliohojiwa.
Mzazi huyo anaelezea uzoefu wake akisema makuzi ya familia za Kiafrika ni tofauti na ilivyo kwa familia za nchi za Magharibi ambazo mara nyingi hukulia katika utamaduni wa namna hiyo.