Wanawake nchni Saudi Arabia rasmi sasa wameruhusiwa kukaa kwenye usukani, baa ya miongo kadhaa kutopata ruhusa hiyo
Mabadiliko haya yalitangazwa mwezi Septemba mwaka jana na Saudi Arabia ikatoa leseni za kwanza kwa wanawake mwanzoni mwa mwezi huu.
Ilikuwa nchi pekee iliyobaki duniani ambapo wanawake walikuwa hawaendeshi magari na familia zao zilikuwa zinakodisha dereva kwa ajili ya wanawake.
Hata hivyo, hatua hii imefikiwa wakati kukiwa na Kampeni ya kuwakamata wanaharakati ambao wamekuwa wakipaza sauti wapatiwe haki ya kuendesha magari.
Takriban wanaharakati wa haki za wanawake wanane wanashikiliwa na huenda wakafikishwa mahakamani na kupatiwa kifungo kwa uanaharakati wao, Shirika la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International limeeleza.
Miongoni mwa wanaoshikiliwa ni pamoja na Loujain al-Hathloul, mwanaharakati kinara katika kampeni hiyo.
Amnesty pia imetaka kufanyiwa mabadiliko makubwa nchini Saudi Arabia, ambapo wanawake bado wameendelea kukandamizwa na sheria zinazowapa mamlaka zaidi wanaume.
Kundi hilo la haki za binaadamu limefanya kampeni kwa miaka mingi kuhakikisha wanawake wanaendesha magari.
Wanawake kadhaa walikamatwa mjini Riyadh mwaka 1990 na baadhi walianza kutuma picha za video wakiwa wamekaa nyuma ya usukani mwaka 2008 na kati ya mwaka 2011 na 2014, Maelfu ta wanawake sasa wataingia barabarani.
Mtangazaji wa televisheni Sabika al-Dosari ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa ''ni tukio la kihistoria kwa kila mwanamke wa Saudi Arabia''.
Amesema alikuwa kwenye usukani mara tu muda wa ukomo wa marufuku ulipotimia.
Hata hivyo, baadhi ya wanaume nchini humo wameelezwa kutoridhishwa kwao na mabadiliko hayo, wakitumia hashtag ya kiarabu ikimaanisha ''Hamtaendesha''.
Kuondolewa kwa marufuku hiyo ni sehemu ya mpango wa Mwanamfalme wa nchini humo,Mohammed bin Salman kubadili mtazamo wa jamii ya Saudi
Hata hivyo bado kuna mambo ambayo wanawake wa Saudi Arabia hawaruhusiwi kufanya,
Wanawake wanapaswa kufuata sheria za nguo wanazopaswa kuvaa, na kutojihusisha na wanaume wasio ndugu zao.Ikiwa wanataka kusafiri, kupata huduma ya kiafya au kufanya kazi, wanapaswa kuongozana mwanaume ambaye ni kiongozi kwenye familia au kuwa na ruhusa yake.