Askofu Dk. Shoo alitoa ufafanuzi huo jana wakati wa ibada uzinduzi wa Dayosisi ya Magharibi Kati ya kanisa hilo mjini Tabora ya kumsimika Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk. Isaac Kissiri na msaidizi wake, Mchungaji Newton Maganga, iliyohudhuriwa na maaskofu wote wa kanisa hilo.
Alisema kanisa linaunga mkono jitihada zote zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Alisema kanisa hilo halina ugomvi na kiongozi yeyote wa Serikali ya Rais Magufuli.
Kuhusu waraka uliotolewa wakati wa Sikukuu ya Pasaka mwaka huu, alisema haukuwa wa kukurupuka na haukutolewa kwa lengo baya dhidi ya Serikali kama baadhi ya watu wanavyoupotosha.
“Naomba kila mpenda amani na maendeleo ya nchi hii aelewe hivyo, waraka huu haukuwa na nia mbaya na Serikali,”alisema Dk. Shoo.
Alisema lengo la waraka huo lilikuwa ni kufikisha ujumbe wa kanisa kwa Serikali iweze kuutafakari na kuufanyia kazi na haukuwa na lengo jingine tofauti.
“Kama kuna sehemu tulieleweka vibaya tuko tayari kuomba radhi kwa nia njema kudumisha ushirikiano mzuri na Serikali.
‘Namshukuru Rais wetu Magufuli kwa kuelewa dhamira yetu, ila wapo baadhi ya watu ndani ya kanisa na nje ya kanisa wasio na nia njema wanaotaka kutuchonganisha na Serikali, watu wa namna hii wasifumbiwe macho, wana agenda binafsi’, alisema Dk. Shoo.
Alisema ndiyo maana maaskofu wote wa kanisa hilo na waumini wao wako kitu kimoja, hawana tofauti zozote.
Kiongozi huyo wa KKKT alionya kuwa mtu anayeendelea kushabikia mambo yanayovuruga amani ndani ya kanisa hilo anakiuka kiapo chake cha utumishi wa Mungu.
Alisema maaskofu wataendelea kushirikiana na Serikali kudumisha amani na utulivu wa nchi na hawako tayari kuona mtu yeyote anatumia jina la kanisa hilo vibaya kwa matakwa yake binafsi kuharibu taswira ya kanisa na Serikali.
“Hatuko tayari kuona mtu anaharibu ushirikiano wetu na Serikali kwa sababu umejengeka muda mrefu, kanisa litachukua hatua kali dhidi yake,”alisema Dk. Shoo.
Alimshukuru Rais Magufuli kukubali mwaliko wao na kumtuma Samia kujumuika nao katika ibada na kuomba awafikishie shukrani za kanisa.