Polisi katika jimbo la Maryland nchini Marekani wanasema watu watano wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulio la risasi lililofanyika katika ofisi za kampuni ya Capital Gazette inayomiliki magazeti ya kila siku katika mji wa Annapolis.
Wafanyakazi wa gazeti hilo wanasema mshambuliaji huyo ambaye ni mzungu anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 ambaye alijiharibu vidole vyake ili kuepusha kutambulika kwa alama za vidole alifyatua risasi hovyo kupitia mlango wa vioo.
William Krampf ambaye ni Msaidizi mkuu wa polisi wa Anne Arundel amesema kwamba wamekuta pia vitu vilivyokuwa na muonekano wa vilipuzi na kuvidhibiti kwa haraka.
Ameongeza kwamba watu zaidi ya 170 waliokuwa katika jengo hilo walisindikizwa na polisi katika kuhakikisha wanakuwa salama kutoka katika jengo hili ambalo pia lilikuwa na biashara nyingine.
Kupitia mtandao wa twiter wanahabari kadhaa waliokuwa katika ofisi hiyo akiwemo Jimmy DeButts ambaye ni mhariri mkuu katika kampuni ya Capital Gazette wameelezea masikitiko yao kufuatia vifo vya wenzao huku wengine wakisema kwamba walikuwa ni kama ndugu zao.