Watanzania Waliokamatwa kwa Uvuvi Haramu Kenya Waachiwa

Serikali imesema Watanzania 109 waliokamatwa hivi karibuni kwa madai ya kufanya uvuvi haramu Bahari ya Hindi, upande wa Kenya wamepata dhamana na kurejea nchini.

Hata hivyo, bado Serikali za pande zote mbili zinaendelea kufanya mawasiliano jinsi ya kulishughulikia suala hilo.

Wavuvi hao walikamatwa eneo la Shimoni, linalomilikiwa na bandari Kusini Mashariki mwa Kenya karibu na mpaka wa Tanzania na kufikishwa mahakama ya Kaunti ya Kwale mwanzoni wa mwezi huu.

Walizuiliwa baada ya kushindwa kulipa dhamana ya Ksh20,000 (sawa na zaidi ya Tsh 450000) kila mmoja.

Tangu wakati huo Serikali ya Tanzania imesema imeanza harakati za kuhakikisha kuwa raia hao wanaachiwa huru.

Akizungumza na gazeti hili leo Juni 27, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Susan Kolimba amesema raia hao waliachiwa na kurejea nyumbani.

“Tayari waliachiliwa baada ya kupewa dhamana wakati mawasiliano ya kiserikali yakiendelea,” amesema naibu waziri huyo kifupi.

Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja tarehe waliyoachiwa  zaidi ya kusisitiza kuwa Serikali inaendelea kujadiliana na Kenya.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad