Watu wawili wanaodaiwa kuhusika na vifo vya simba tisa waliolishwa sumu katika Kijiji cha Nyichoka wilayani hapa wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Waliofikishwa mbele ya hakimu wa Mahakama hiyo ni Mwikwabe Chacha na Mhoni Waisaya wote wakazi wa Kijiji cha Nyichoka, Kata ya Kyambahi.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Emmanuel Zumba aliiambia Mahakama kuwa Mei 30 mwaka huu katika eneo la Nyichoka watuhumiwa hao waliwaua simba tisa wenye thamani ya Sh97 milioni.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 35 ya mwaka 2018; Mwendesha mashtaka Zumba aliiambia Mahakama hiyo kuwa washtakiwa waliwatega simba hao kwa kuwawekea sumu kwenye mzoga wa ng’ombe.
Alisema kwamba kosa hilo ni kinyume cha kifungu namba 86 cha Sheria ya Wanyamapori Namba Tano ya mwaka 2009.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote na wamerudishwa mahabusu kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa dhamana kwa kesi kama hizo zenye thamani ya zaidi ya Sh10 milioni, hivyo wanatakiwa kuomba dhamana Mahakama Kuu. Kesi hiyo itatajwa tena Juni 26 mwaka huu.
Mei 31 mwaka huu mizoga ya simba ilionekana huku mmoja akiwa amekatwa miguu na mkia na mwingine ametolewa ngozi ya mgongoni na watu wasiojulikana.
Kikosi cha kuzuia Ujangili Kanda ya Serengeti na kamati ya Ulinzi ya Kijiji cha Nyichoka walifanikiwa kuwakamata watu saba na baada ya mahojiano watu wawili ndiyo wamefikishwa mahakamani.