Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Afungua Mashindano Ya Umisseta Na Umitashumta- Mwanza


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Elimu wahakikishe wanafunzi wanaoshiriki mashindano hayo ni wale waliovuka katika ngazi ya shule, kata, wilaya na mkoa, ambao wote ni wanafunzi halali wa shule na marufuku kuchezesha mamluki.


“Endapo itabainika yupo mchezaji aliyeletwa kushiriki michezo hii ambaye si mwanafunzi (yaani mamluki) naagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika kwa kuzingatia kanuni na sheria za mashindano haya,” amesisitiza.


Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Juni 9, 2018) wakati akifunguaMashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari Tanzania yanayofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.


Pia, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mikoa na wilaya zote nchini wahakikishe kuwa masomo ya haiba, michezo na stadi za kazi yanafundishwa kikamilifu kwenye shule zote za msingi.


Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema somo la elimu ya michezo kwa Shule za Sekondari nalo lifundishwe kikamilifu na vyuo vya michezo kama Malya viendelee kuwaendeleza walimu wa michezo.


Amesema utafiti na ubunifu wa kuendeleza michezo nchini ni jambo linalohitaji kupewa msukumo wa pekee, ambapo ameviasa vyama vya michezo na asasi za sanaa zijihusishe na ukuzaji wa michezo shuleni, bila kuathiri taratibu za shule.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaagiza Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe maeneo ya michezo na burudani yanapimwa na yasiingiliwe, pia vitengo vya michezo kwenye ofisi za Halmashauri na Mikoa vitengewe fedha za kuendeshea michezo.


Amesema pamoja na manufaa yatokanayo na michezo, kiwango cha michezo  nchini si cha kuridhisha, hivyo  ni vema kujenga msingi wa kupata matokeo mazuri kwa kuwa na viwanja vyenye viwango vinavyokubalika, walimu wenye utaalamu wa michezo na vifaa.


“Inawezekana kuna sababu za msingi, lakini ni lazima tuhakikishe kuwa vijana kuanzia Shule za Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo wanatengenezewa mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na kupewa fursa za kucheza na kushindana miongoni mwao,” amesema.


Amesema kutokana na hali hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kupitia shule za msingi na sekondari, itahakikisha walimu waliosomea michezo wanapata ajira ili waendeleze vipaji vya vijana nchini.


Waziri Mkuu amesema vipaji vya michezo na sanaa vitaitangaza nchi kimataifa na kuongeza fursa ya ajira kwa Watanzania. Amesema kauli mbiu ya michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA ya mwaka  huu ni “michezo, sanaa na taaluma ni msingi wa maendeleo ya mwanafunzi  katika Taifa letu”.


Amesema kauli mbiu hiyo inawataka wanafunzi wajihusishe na michezo na sanaa kama sehemu ya taaluma, ambapo wataweza kuonesha vipaji vyao ambavyo vikiendelezwa vema vitawapatia manufaa ikiwemo afya, matokeo mazuri ya kitaaluma na ajira.


Pia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella na wananchi wote kwa kukubali kuwa wenyeji wa mashindano hayo kwa mara ya tatu mfululizo, pamoja na  kampuni ya COCA COLA kwa kudhamini michezo ya mpira wa miguu na kikapu kwa Shule za Sekondari na kampuni ya AZAM kwa kujitolea kuonesha michezo hiyo kwa mwaka huu.


Aidha, amewataka wanafunzi wanaoshiriki mashindano hayo watumie ushiriki wao kwa kuuthibitishia umma dhamira waliyonayo ya kuonesha kuwa, zipo fursa nyingi za ajira endapo vipaji vya michezo na sanaa vitatumika kikamilifu.


Amesema mashindano kama hayo yanatoa fursa kwao kuonesha uwezo wao na kuonekana kwa wadau mbalimbali  wanaoweza kuwaendeleza.  “Si hivyo tu, uwepo wenu hapa unawapa fursa ya kutambua uwezo mlionao pamoja na kujiwekea malengo na mwelekeo wa maisha yenu ya baadaye,”.


Amesema uhalali wa michezo na mashindano shuleni unatajwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020, Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995,  Sera ya Elimu ya mwaka 2014 ambazo kwa pamoja zinaelekeza kutambua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi shuleni kufikia malengo ya maendeleo endelevu.


Mashindano hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri waNchi, OR – TAMISEMI, Joseph Kakunda, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, Wadhamini wa Mashindano hayo, Wadau wa michezo na baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mwanza.


IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad