SERIKALI imesema hairidhiki na ubia unaoendeshwa kwenye Kiwanda cha Nguo cha Urafiki.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo jioni (Ijumaa, Juni mosi, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wafanyakazi wa kiwanda hicho mara baada ya kukagua mitambo mbalimbali kwenye kiwanda hicho.
“Serikali haturidhiki na ubia huu, na huyu mbia aelewe kwamba Serikali haturidhishwi na ubia huu wala kinachoendelea hapa kiwandani,” amesema huku akishangiliwa kwa nguvu na wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bw. Charles Mwijage aongoze kikao baina ya wabia hao na menejimenti ya kiwanda na apewe taarifa hiyo leo saa 12 jioni baada ya kufuturu.
“Ubia wenu hauna tija. Kwa hiyo wewe Msajili wa Hazina na huyo mwekezaji, nikitoka hapa, mbaki mfanye kikao na mnipe majibu leo saa 12 jioni. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Mkuu wa Mkoa muongoze mjadala huo na nikitoka kufuturu mniambie maazimio yenu, na kama haiwezekani, mvunje kabisa ubia huo ili tujue hatuna mbia tutafute mbia,” amesema.
Waziri Mkuu amesema wabia wakuu wa kiwanda hicho ni Msajili wa Hazina na kampuni ya Changzhou State owned Textile Assets Operations kutoka China na kwamba Serikali ilipoamua kukaribisha uwekezaji ilitarajia kupata mtaji, teknolojia na ajira za kutosha lakini hali ya sasa ni kinyume kabisa.
“Hatuwezi kuvumilia, tunasema tuna mbia mwenye mtaji, hakuna mtaji; tulisema tunataka mbia mwenye kuleta teknolojia mpya, hakuna teknolojia; tulisema aendeshe shughuli hii kukiwa na ajira endelevu, hizo ajira hakuna; halafu tubaki tunamwangalia tu. Bora atuambie amekwama, aondoke, tutangaze vinginevyo,” amesema.
“Tulikopa mtaji lakini Tanzania hizo hela hazijaja, tunataka majibu ya fedha hizo; kama fedha iliyokopwa kwenye Benki ya Exim ya China ingeletwa nchini tungeweza kuziba mapengo na kusaidia kiwanda kiweze kufanya kazi. Sasa kwa sababu fedha hiyo haijaja nchini, tunataka maelezo fedha hiyo iko wapi?” amesisitiza.
“Mitambo iliyonunuliwa na mwekezaji miaka mitano au sita iliyopita haifanyi kazi tangu ilipoletwa nchini, nataka majibu, je mitambo hii ilinunuliwa ikiwa mizima au vipi; na tena mmeng’oa mashine kwenye ma-godown matatu, nimeambiwa mlikuwa na nia ya kuleta mashine mpya, lakini sasa ni miaka mitano, je mashine zile zote zimeenda wapi, na kama mmeuza ameuziwa nani? Mkae mjadili na leo hii mniletee majibu yote haya,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema kiwanda hicho ni matokeo ya urafiki wa China na Tanzania na kina historia ndefu na mahusiano ya muda mrefu. “Asiingie mtu akatuharibia, na tunataka mahusiano yetu na China yaendelee. Amesema baada ya kupokea taarifa hiyo, Serikali itakaa na Balozi wa China ili itafutwe suluhisho.
Waziri Mkuu amewataka watumishi wa kiwanda hicho walioko likizo na wale waliopo kazini wawe wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutafuta dawa ya matatizo yao.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemtaka Meneja Rasilmali Watu na Utawala wa kiwanda hicho, Bw. Edwin Nkwanga aandae orodha ya watumishi wote yenye kuonyesha kila mtumishi analipwa nini na aifikishe kwake haraka.
“Hapa kuna watu wanalipwa sh. milioni saba hadi 10 na wengine wanalipwa sh. 120,000. Niletee orodha yenye kuonyesha jina, cheo na kiwango cha mshahara, lakini pia uonyeshe anapata stahili zipi, kama ni posho ya nyumba, maji au umeme,” amesema.
Amesema nia ya Serikali ni kutaka kupanga upya mishahara yao ili waweze kupatikana watumishi wa kutosha.
Wakati akikagua kiwanda hicho, Waziri Mkuu alielezwa kwamba kuna mashine 88 ambazo ziling’olewa kwenye kiwanda hicho na hazijulikani zimepelekwa wapi.
Mapema, akitoa taarifa fupi ya kiwanda hicho, Naibu Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Shadrack Nkelebe alisema kiwanda hicho kimesimamisha uzalishaji tangu Desemba 2017 ili kufanya ukarabati na kimeshindwa kuendelea nao kwa sababu ya madeni.
“Kiwanda kilikuwa na watumishi 3,000 lakini sasa hivi wamebakia 726 baada ya wengine kupunguzwa na kulazimishwa kwenda likizo licha ya teknolojia kubakia ni ileile. Kiwanda kinakabiliwa na changamoto nyingi lakini kwa sehemu kubwa ni za kutengeneza. Tumepigana vita katika kujenga uchumi wa Taifa kupitia kiwanda hiki, lakini tumekwama. Tunahitaji nguvu ya ziada ili tutoke hapa,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU