SERIKALI imesema itaongeza nguvu kuhakikisha wagonjwa wa figo, moyo na saratani wanapata huduma za kibingwa katika hospitali za hapa nchini.
Pia imesema haitamvumilia mtu yeyote ambaye atasababisha kudorora kwa mkakati huo wa serikali wa kuwezesha huduma za magonjwa yasiyoambukiza nchini ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini hapa. Bodi hiyo inaongozwa na Dk Deodatus Mtasiwa.
“Mimi nitaendelea kuwa mkali sana kwa mtumishi yeyote atakayesababisha kudorora au kukwama kwa huduma za afya katika hospitali zetu,” alisema Ummy na kuitaka bodi hiyo kuwa makini na kuhakikisha hakuna uzembe unaofanyika katika uendeshaji wa hospitali hiyo nyeti.
Alisisitiza kuwa usimamizi makini utawezesha lengo la kuanzishwa kwa hospitali hiyo la kutoa huduma za afya maalumu za kibingwa, huduma za uchunguzi na tiba kwa magonjwa yote huku ikijikita zaidi kwenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama figo, moyo, macho, damu na saratani kufikiwa kwa ufanisi uliotarajiwa.
Huduma nyingine zilizopangwa kutolewa ni pamoja na kutoa huduma za endoscope, kufundisha wataalamu wa kada za afya na kufanya tafiti mbalimbali ili kuboresha afya ya jamii ya Watanzania na hivyo kuipunguzia serikali mzigo wa gharama za matibabu nje ya nchi.
Akizungumzia umuhimu wa hospitali hiyo, alisema kuna ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza duniani kwani Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema wagonjwa 100, kati ya hao, 47 huugua magonjwa yasiyo ya kuambukiza, na vifo 100, kati yake, 60 hutokana na magonjwa hayo.
“Kama tusipochukua hatua za kudhibiti takwimu hizo zitaongezeka mara mbili zaidi na serikali itaongeza nguvu kusaidia magonjwa ya figo, moyo na saratani,” alisema Ummy.
Alisema kwa mwaka 2013 hadi 2016, serikali ilipeleka wagonjwa 590 kwenda kutibiwa nje ya nchi, ambao wagonjwa 430 kati yao, walikuwa wa moyo na 160 wa kupandikizwa figo.
“Kwa takwimu za kuanzia Julai 2013 hadi Juni 2016, magonjwa ya moyo na figo ndiyo yalikuwa yakiongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa kutibiwa nje ya nchi na kuigharimu serikali kiasi cha shilingi bilioni 36.6,” aliongeza waziri.
Alisema, kati ya wagonjwa 590 waliosafirishwa na serikali, 430 walienda kutibiwa moyo na 160 walienda kupandikizwa figo.
Alisisitiza kuwa kwa kuanzishwa huduma hizo katika hospitali mbalimbali nchini ikiwemo ya Benjamin Mkapa, kutaokoa kiasi kikubwa cha fedha na kuipunguzia serikali mzigo wa gharama.
Aliiagiza Bodi ya Hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa kwa kuwa imeanza upandikizaji wa figo kuhakikisha inaweka malengo ya kupandikiza idadi maalumu ya wagonjwa itakayosaidia kukuza uwezo na taaluma.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Alphonce Chandika alimweleza waziri kwamba baada ya mafanikio ya upandikizaji wa figo wakisaidiana na wadau wa Tokushukai kutoka Japan, Machi 22, mwaka huu, wagonjwa wengine watafanyiwa upandikizaji huo Agosti mwaka huu.
Alisema mwezi ujao wataanzisha upasuaji wa kutumia matundu madogo kwa kushirikiana na wadau kutoka Marekani baada ya madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, koo, pua na masikio kurejea nyumbani wakitokea India walikonoa bongo zao kuhusu tiba hiyo.
Pamoja na kutaka usimamizi makini ili kuokoa maisha ya Watanzania na fedha zinazotumika kupeleka wagonjwa nje, Ummy alitaka bodi kuhakikisha fedha za mkopo Sh bilioni 119 kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zilizokopwa kujenga hospitali zinalipwa.
Akizungumzia masuala ya utafiti, pamoja na kulazwa kwa wagonjwa, alisema ndani ya mwezi moja wagonjwa wataanza kulazwa katika hospitali hiyo na anatarajia watakaofika kulazwa ni wale wanaohitaji huduma za kibingwa.
“Ndugu Mwenyekiti wa Bodi, tafiti ni eneo nyeti na muhimu sana katika kukuza na kuendeleza weledi, ujuzi na maarifa katika taaluma mbalimbali, hivyo ni lazima hospitali ijikite katika kufanya tafiti mbalimbali ili kugundua matatizo/changamoto na kuyapatia majawabu kwa maendeleo ya hospitali na Taifa kwa ujumla,” alisema Ummy.
Aliongeza kuwa ni matumaini yake bodi hiyo kwa kushirikiana na uongozi wa hospitali itahakikisha shughuli za utafiti zinaendelea kufanyika kikamilifu na matokeo ya utafiti yatumike kubaini na kutatua changamoto ili kuboresha utoaji wa huduma ya matibabu nchini.
Alisema uanzishwaji wa hospitali hiyo ya kibingwa ni utekelezaji wa mikakati ya serikali ya kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.