Klabu ya Yanga wanatarajia kuweka bayana majina ya wachezaji watakaobaki katika kikosi hicho na wale watakaoachwa huku pia wakitangaza maingizo mapya ndani ya kikosi hicho.
Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu hiyo Hussein Nyika ameeleza hayo huku akisisitiza kuwa staili yao ya kusajili ni ile ile ya kimya kimya na hawataki kuonesha tambo zozote.
"Tunasajili kimya kimya na mambo yetu yote yatakuwa hadharani pindi kocha wetu atakaporejea kutoka Ufaransa, kila kitu kinaenda sawa na watu wawe watulivu", amesema Nyika.
Nyika ameongeza "Kuhusu wachezaji wetu waliomaliza mikataba tupo katika harakati za kuwaongeza kama kocha bado atakuwa na matumizi nao na akarudi tutatangaza wanaobaki na watakaopelekwa klabu zingine kwa mkopo".
Yanga wanajiandaa na mchezo wa hatua ya makundi katika kombe la Shirikisho barani Afrika huku wakitarajia kukipiga na Gor Mahia ya nchini Kenya Julai 18 mwaka huu.