YANGA sasa imeamua. Katika kinachoonekana kama ni kumjibu bilionea wa Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji, Kamati ya Usajili ya Yanga sambamba na ile ya vigogo 12 imeanza kujadili usajili wa kiungo fundi wa Simba, Said Ndemla ili atue Jangwani.
Hata hivyo, hatma ya Ndemla kutua Yanga inategemea na maamuzi ya mwisho ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera anayesubiriwa arejee kutoka Ufaransa, ingawa tayari mabosi wawili walio nje ya kamati zote za Yanga kumaliza kazi mapema.
Ndemla hajasaini mkataba mpya na Simba mpaka sasa huku mazungumzo yakiyumba kutokana na kiungo huyo kuweka dau kubwa mezani mwa mabosi wake wa sasa na pia akiwa anaona kubaki Msimbazi ni kama kupoteza muda wake bure.
Kinachomchanganya Ndemla kwa mujibu wa chanzo makini kutoka ndani ya Yanga ni kiasi kikubwa cha ofa aliyopewa na Yanga ambayo ni mara mbili kulinganisha na ile aliyopewa na Simba.
Yanga wanatafuta kiungo mchezeshaji na akili yao wanaona Ndemla sio mbaya akipatikana lakini maamuzi kamili akaachiwa Zahera aweze kuamua kipi kitamfaa kutoka kwa kiungo huyo.
Usajili wa Ndemla upo mikononi mwa vigogo wawili ambao akili yao inataka kufanya mambo kwa weledi, lakini kama wakipata ruhusa basi watahakikisha wanapeleka jina la kiungo huyo Jangwani huku Simba ikiwa kilio.
Mwanaspoti linafahamu Simba imemwekea mezani kiasi cha fedha kisichozidi Sh40 milioni, lakini kiungo huyo alipovuka mtaa wa pili akaambiwa utachukua zaidi ya hiyo kama uko tayari sema tupeleke jina lako Ufaransa aliko Zahera kwa sasa ili atupe jibu kamili.
Mwanaspoti ndio wa kwanza kubandika habari ya Ndemla kutakiwa na Yanga kabla ya Ligi Kuu Bara mzunguko wa kwanza kumalizika.
Jana Mwanaspoti lilirudi kwa Ndemla katika kujua ukweli wa hilo alisema mkataba wake na Simba umeshamalizika na anachosubiria ni kukaa mezani na mmiliki wa klabu hiyo Bilionea Kijana Mohammed Dewji ‘MO’ na si kuongea na mtu yeyote wa kati.
“Nimemaliza mkataba nikiwa na Simba na naimani wameelewa huduma yangu niliyokuwa nikiwapa kipindi chote nikiwa hapa na sitasaini mkataba kokote mpaka nitakoposhindwana na Simba,” alisema.
“Naimani nitakutana na MO na tutaongea na kumalizana kuhusu mkataba mpya, lakini kuhusu Yanga, siwezi kusema kama wamenifuata au hawajanifuata ni jukumu la wakala wangu,” alisema Ndemla.
Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya kuivusha Yanga katika kipindi cha mpito, Tarimba Abbas alifunguka akidai baadhi ya nyota wa klabu hiyo ni mizigo na hawana hadhi, hivyo watafanya usajili wa kimya kimya kuisuka Yanga ya Kimataifa.
Tarimba alisema kwa sasa wapo katika harakati za kutafuta wachezaji watakaoweza kurejesha heshima ya timu hiyo baada ya kupoteza ubingwa msimu huu kwa watani zao Simba wanaotambia fedha za mwekezaji wao, Bilionea Mohammed Dewji.
“Kwa sasa tuna wachezaji wengi ambao wanashindwa kuleta matokeo mazuri, klabu yetu imekuwa kubwa zaidi yao, tuna jukumu la kufumua kikosi hicho na kuhakikisha tunasajili nyota wa kurejesha faraja kwa klabu, zoezi ili litafanyika kwa kushirikiana na Kamati ya Usajili, benchi la ufundi na wadau wengine wanaoitakia mema Yanga.”
Tarimba alisema wamekuja na staili ya kumfukuza mwizi kimya kimya katika kufanya mambo ya usajili na wanafanya hivyo kutokana na tabia ya baadhi ya timu kuwasajili wachezaji ambao walikuwa katika rada zao.
“Tunahitaji kuwa na timu ambayo itacheza soka na kuleta matokeo hata kama baadhi ya wachezaji wana matatizo, tunataka kuona kocha mkuu anakuwa na kikosi kipana ambacho kitafanya vizuri katika mashindano yoyote,” alisema.
Aidha Tarimba alisema kujitoa kwao kwenye michuano ya Kombe la Kagame ni sahihi kwa sababu ni vigumu kushiriki katika mashindano hayo ambayo hayakuwepo katika Kalenda ya Soka.
Alisema Yanga, Simba, Singida na JKU zilijua mapema mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara, kutakuwa na mashindano ya SportPesa Super Cup nchini Kenya kutokana na umakini waliokuwa nao.
“Michuano hii haikuwepo katika mwezi uliopangwa na hata Yanga haikujua ili kuweka mikakati ya usajili mapema, kwa sasa wachezaji wengi hawana mikataba na wapo likizo, ni vigumu kufanya mambo hayo makubwa mawili kwa mpigo,” alisema.