Uongozi wa Klabu ya Yanga umeendelea na msimamo wake wa kutoshiriki mashindano ya vilabu Afrika Mashariki, maarufu kama kombe la Kagame, kwa lengo la kujiandaa na michuano ya vilabu Barani Afrika.
Akiongea na www.eatv.tv leo Juni 12, 2018 katibu mkuu wa Yanga, Bwana Charles Boniface Mkwasa, amesema kwamba klabu hiyo iliandika barua kwenda kwa TFF kueleza lengo la kujitoa katika mashindano hayo na haitaweza kubadili msimamo na kuongeza kuwa barua yao haijajibiwa.
“Sisi tulishapeleka barua na hatujapata barua yoyote kutoka kwa TFF kutaka kitu chochote, hatuwezi kuambiwa kupitia televisheni au vyombo vya habari, tunaambiwa kupitia barua rasmi kama sisi tulivyopeleka barua, hata hivyo hakuna mabadiriko yoyote” amesema Mkwasa.
kwa upande wa msemaji wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Bwana Clifford Ndimbo amesema Shirikisho hilo litatoa taarifa rasmi kuijibu barua ya Yanga pasipo kutaja ni baada ya muda gani.
“Yanga waliandika barua ya kujitoa, ambayo tuiliipokea na tukasema tutakuja kutolea ufafanuzi, hatujajua lini tutakuja kutolea ufafanuzi, huwezi kulazimsha shirikisho likuambie leo, kila taasisi ina utaratibu wake” amesema Ndimbo.
Juni 8, 2018 uongozi klabu ya Yanga uliandika barua kwa TFF ya kujitoa katika mashindano ya Kagame Cup yatakayoanza Juni 29 mpaka Julai 13, 2018 Jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho la vilabu Barani Afrika.