Zitto Kabwe Ajitosa Kuwapigania Wakulima wa Korosho Kwa Kupinga Marekebisho ya Sheria Mpya ya Zao Hilo

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema chama hicho kitashirikikiana na wabunge wa vyama vya upinzani kupinga marekebisho ya Sheria ya Sekta ya Korosho namba 203.

Jana Jumatano Juni 20, 2018, Zitto ametoa taarifa katika mitandao mbalimbali ya kijamii akipinga mabadiliko hayo, kutaka wananchi kukataa kile alichokiita dhuluma kwa wakulima wa korosho.

Zitto ametoa kauli hiyo wakati Serikali ikikusudia kuifanyia marekebisho sheria hiyo.

Kwa mujibu wa muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2018, inapendekezwa kufutwa mgawo wa fedha zinazotokana na ushuru wa kusafirisha korosho nje zilizokuwa zikitolewa kwa wakulima ili kuboresha zao hilo.

Badala yake, muswada unapendekeza fedha hizo kupelekwa mfuko mkuu wa Hazina kama fedha nyingine za Serikali.

Sheria ya sasa inataka asilimia 65 ya fedha zinazotokana na ushuru wa kusafirisha korosho nje kupelekwa kwa wakulima kupitia Bodi ya Korosho (CBT).

"Sisi ACT Wazalendo, kwa kushirikiana na wabunge wote wa upinzani, pamoja na wale wa CCM watakaokuwa tayari kuwatetea, tutajitahidi sana kuhakikisha mapendekezo haya hayapiti,” amesema Zitto katika taarifa yake hiyo, akiwaeleza wananchi kuhusu mabadiliko hayo.

"Lakini Kuna haja kubwa ya wananchi, wakulima wa korosho, hasa wa mikoa ya kusini, kupaza sauti kukataa. Tusikubali.”

Amesema katika marekebisho hayo Serikali inapendekeza kufuta mgao wa fedha zinazotokana na ushuru wa kusafirisha korosho nje, “katika mgao wa sasa wa fedha hizo Serikali huchukua asilimia35 ya fedha, na asilimia 65 inayobakia hupelekwa kwenye mfuko wa kuendeleza zao la korosho nchini.”

“Fedha hizo kuingizwa mfuko mkuu wa Hazina kama fedha nyingine za Serikali, na hivyo kutumika kwa asilimia 100 kwa mambo mengine na sio kwaajili ya kuendeleza zao la korosho.”

Amedai  Serikali imegoma kutoa asilimia 65 ya uendelezaji korosho na imeshazitumia fedha za Korosho Sh211bilioni  kinyume cha sheria ya sasa.

“Wameamua sasa kufuta hiyo sheria ya korosho kabisa ili wasibugudhiwe. Tutapambana bungeni kupinga dhuluma hii dhidi yenu, ikishindikana tutarudi kwenu,” amesema.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad