Lile sakata la serikali kuliandikia barua Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, (KKKT) limezua mjadala kwenye twitter za viongozi mbalimbali wa kisiasa.
Jana Juni 6, mara baada ya kusambaa kwa barua hiyo inayodaiwa kuandikwa Mei 30 na Wizara ya Mambo ya Ndani ikilitaka KKKT kuufuta waraka wa maaskofu, viongozi wa kisiasa walianza kutuma ujumbe kwenye akaunti zao za twitter.
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe ameandika katika ukurasa wake akisema: “Tishio la serikali kwa kanisa la KKKT linapaswa kupingwa na kila mtanzania. Tukiruhusu KKKT kuingiliwa, hakuna atakayepona.”
Jana jioni, Zitto aliandika tena na safari hii alipeleka ujumbe moja kwa moja kwenda kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, wa CCM, Humphrey Polepole akisema:
“Nimeambiwa kuwa TEC ya Kanisa Katoliki pia imepewa barua kama ya KKKT. Serikali ya CCM ya awamu ya Tano imeamua kupambana na makanisa 2 makuu nchini ...”
Baada ya kutumwa kwa ujumbe huo na Zitto, Polepole amejibu akisema:
“Serikali makini ina wajibu wa kukumbusha, kuelekeza, kuonya au kuchukua hatua kwa mtu/taasisi yoyote inayokwenda kinyume na taratibu za nchi ambazo tumejiwekea. Nimeisoma barua ya Msajili anazo hoja za msingi. Usijichomeke hapa kutafuta huruma na umaarufu hewa. Soma Warumi 13:1-5.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent Mashinji yeye ameandika akisema:
“Nimeona barua hii kwa masikitiko na majonzi makubwa. Naweza sema tu kwamba: “hakuna mtu mwenye akili timamu aliyewahi kuvunja kioo kilichomwonyesha uchafu wake.”