Baada ya kuwepo kwa mashinikizo mbalimbali yakimtaka Freddy Lowassa kijana wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Mh. Edward Lowassa, kugombea nafasi ya Ubunge kwenye jimbo la Monduli. Mh. Lowassa amesema bado hajawa na maoni juu ya mashinikizo hayo kwani hayajamfikia.
Mh. Lowassa ameyasema hayo wakati alipohojiwa kama yupo tayari kumruhusu kijana wake Freddy Lowassa kuchukua dhamana ya kuiongoza Monduli baada ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Julius Kalanga kujiuzulu nafasi yake .
Mh. Lowassa amesema; "Mimi bado taarifa hizo za kumhusu Freddy sina, sijazipata. Ngoja kwanza nizifuatilie na baada ya hapo ninaweza kutoa tamko. Siwezi kuzungumzia kitu kwa sababu bado mimi hazijanifikia,".
Tangu kusambaa kwa taarifa za Mbunge Kalanga kujiuzulu nafasi yake na kuhamia CCM jana usiku, mitandaoni kumekuwa na mashinikizo mbalimbali ambayo yakimtaka Freddy Lowassa kuwa mwakilishi wa wanaMonduli huku wakidai kwamba Kalanga amewaambisha wamasai.
Mmmojawapo ya watu hao ni Mbunge wa Sombetini Arusha, Ally Binamu Bananga yeye amedai kwamba yeye atakishawishi chama kimpitishe Freddy kugombea.
"Huyu ndio wa kwenda kuzima kiherehere cha Kalanga, uchaguzi mdogo ukiitishwa nitakishawishi chama changu twende na FREDDY LOWASSA, kampeni meneja nakamata ungo mwenyewe mzee baba, mkuu wa ngome Godbless Lema, huku mzee Lowassa, kule mama Lowassa" , ameandika Bananga ujumbe huo.
Jimbo la Monduli limekuwa wazi kuanzia jana usiku baada ya Mbunge aliyechaguliwa 2015 (CHADEMA), Julius Kalanga kujiunga na CCM kwa kile alichoeleza kuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli na kudai kuwa ameondoka CHADEMA kwasababu ya siasa za chuki na uhasama.