Aliyetoroka Chini ya Ulinzi Adakwa

Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linamshikilia Mwapulise Mfikwa (28), aliyetoroka chini ya ulinzi katika Mahakama ya Wilaya ya Njombe akiwa anakabiliwa na shtaka la mauaji.

Mtuhumiwa huyo alinaswa juzi saa mbili usiku akiwa kijiji cha Ngomai, Wilaya Kongwa, mkoani Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Gilles Muroto, alisema mtuhumiwa huyo alitoroka akiwa chini ya ulinzi katika mahakama hiyo Juni 12, mwaka huu akikabiliwa na shtaka la mauaji.

“Mshtakiwa baada ya kutoroka alijificha shambani Kiteto mkoani Manyara na kijiji cha Ngomai, Wilaya ya Kongwa,” alisema.

Alibainisha kwa kuwa taarifa za kutoroka kwake zilienea maeneo mengi jijini hapa, watu wasiopenda uhalifu walifanikisha kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha Kituo cha Polisi Kibaigwa.

“Nawapongeza wananchi waliofanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyu hatari, na pia aliwahi kufungwa jela kwa kosa la kupatikana na silaha,”alisema.

Alisema mtuhumiwa huyo atasafirishwa kwenda Njombe kuendelea na shtaka lake la mauaji na kufunguliwa jipya la kutoroka chini ya ulinzi.

Hata hivyo, alisema Dodoma na maeneo jirani yataendelea kuwa salama kama ushirikiano huo utaimarishwa katika kupambana na wahalifu waliomo katika mitaa wanayoishi.

“Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linawashukuru wananchi na linawapongeza kwa dhati kwa ushirikiano wao mzuri katika kupambana na uhalifu na wahalifu,”alisema Muroto.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad