Gari la kubeba wagonjwa (ambulance) la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mara, limekamatwa likiwa na shehena ya dawa za kulevya aina ya mirungi.
Akizungumzia tukio hilo leo, Julai 11, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema gari hilo lilikamatwa jana Julai 10, wilayani Bunda.
"Dereva wa gari hilo aliitwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kubeba mgonjwa usiku wa jana lakini alisema yupo mbali na gari halina mafuta,” amesema Malima.
Malima amesema dereva huyo alitakiwa kumsafirisha mgonjwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Akifafanua zaidi Malima amesema baada ya dereva kutoa udhuru, mgonjwa aliyehitaji huduma ya rufaa alisafirishwa kwa kutumia gari la polisi.
“Lakini gari la polisi likiwa njiani kuelekea jijini Mwanza, waliokuwamo ndani ya gari hilo waliiona ‘ambulance’ inayodaiwa kutokuwa na mafuta ikiwa eneo la Bunda.”
"Askari polisi na maofisa wengine waliokuwamo kwenye gari la polisi walilazimika kulisimamisha lile gari la wagonjwa kujua lilikotoka na linakoelekea ndipo wakamkuta dereva ambaye awali alidai gari halina mafuta ndipo walipokuta limesheheni shehena la mirungi,” amesema
Amesema dereva yule hakuwa na la kujitetea ndipo alipotiwa mbaroni na anaendelea kushikiliwa kwa mahojiano,"
Mkuu huyo wa mkoa amesema taarifa zaidi kuhusu tukio hilo la aina yake kuwahi kutokea mkoani Mara zitatolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe.