Mbunge wa kuteuliwa, Anne Kilango Malecela amejiteua kuwa mbunge wa Jimbo la Moshi mjini ili kukamilisha muundo wa uongozi aliouita wa mafiga matatu katika kushughulikia kero za wananchi.
Kilango ambaye ni miongoni mwa wabunge wa kuteuliwa na Rais John Magufuli, ametengaza uamuzi huo katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea udiwani kata ya Mawenzi kwa tiketi ya (CCM) Apaikunda Naburi.
"Mafiga matatu ndiyo yanayopika ngoja niwaambie leo watu wa Mawenzi, na asiwadanganye mtu, tupeni diwani wa CCM ili kukamilisha mafiga matatu,mtauliza mbunge ni nani? mbunge ndio mimi hapa”, amesema Kilango.
Kilango amesema mafiga matatu ndio yanayopika chakula akitaka kuwepo na sare ya kuwepo Rais anayetokana na CCM, mbunge anayetokana na chama hicho sambamba na diwani.
Akiomba kura katika mkutano huo, Apaikunda amesema yeye ndio anazifahamu vizuri kero za wananchi wa kata hiyo likiwamo tatizo la taa za barabarani na maeneo ya kufanyia biashara kwa machinga, hivyo akaomba wamchague ili kuzipatia majawabu kero hizo.
Jimbo la Moshi mjini linaongozwa na mbunge kutoka upinzani, Jafary Michael ambaye ni kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).