Askari Mwingine Ajiua kwa Kujipiga Risasi Kisa Wivu wa Mapenzi

Askari Mwingine Ajiua kwa Kujipiga Risasi Kisa Wivu wa Mapenzi
ASKARI Polisi, Constebo Nelson William, amejiua kwa kujipiga risasi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za wivu wa mapenzi.

Tukio la askari huyo kujiua ni la pili ndani ya siku mbili baada ya askari mwingine wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Tabora, Michael Hosea, kujipiga risasi shingoni na kutokea utosini.

Kutokana na mfululizo wa matukio hayo,  Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, ameelezea kushtushwa kwake huku akiwaomba viongozi wa dini nchini kuendelea kufanya doria za kiroho, wakati jeshi hilo likiendeleza doria za kimwili.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki, alisema askari huyo alijipiga risasi juzi majira ya saa 8:30 mchana akiwa eneo la kambi za polisi alikokuwa anaishi.

Kamanda Ndaki alisema kuwa kabla ya kujipiga risasi, William aliacha ujumbe kuwa ameamua kujiua kutokana na wivu wa mapenzi kwa kuwa amekuwa hana uhusiano mzuri na mpenzi wake.

Alisema kabla ya kuchukua uamuzi huo, askari huyo aliingia kwenye malumbano na mpenzi wake baada ya kwenda kwenye chumba cha mpenzi wake huyo na kisha kuamua kuharibu mali alizonunua.

Ndaki alisema baada ya tukio hilo la kuharibiwa mali, mwanamke aliamua kwenda kutoa taarifa polisi, kitendo ambacho William hakikumfurahisha kwa madai kuwa aliona kama amedhalilishwa.

Kutokana na kitendo hicho, Kamanda Ndaki alisema William aliona njia pekee ni kuchukua uamuzi wa kujiua na ilipofika muda huo akaamua kujipiga risasi.

Alipoulizwa kama kuna mtu yoyote amekamatwa, Kamanda Ndaki alijibu hakuna kwa kuwa askari huyo ameacha ujumbe kuwa amejiua kwa sababu ya wivu wa kimapenzi.

Ndaki alisema kwa sasa mwili wa askari huyo umehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti wakati taratibu za mazishi zikiendelea.

Alisema mwanamke huyo alikuwa akiishi kwenye chumba chake alichopanga wakati William alikuwa akiishi kambini.

Katika ujumbe alioacha, William alieleza mambo mengi na kutaka ujumbe huo usomwe siku ya kuuaga mwili wake.

Ujumbe alioacha marehemu ulisomeka hivi:

“Mimi Nelson William Mkonda, nimeamua kuchukua uamuzi wa kujiua kwani niliyekuwa na uhusiano naye, Amina Adam Bakari, niligombana naye siku mbili zilizopita.



“Nimefanya uharibifu wa kuvunja vyombo vya ndani ambavyo asilimia kubwa ni vyombo vyangu. Amenilipisha Sh. 1,500,000 ambapo mimi roho yangu imeuma sana na pesa hiyo nimekopa kwa mtu, naomba arudishe yeye mwenyewe hizo pesa.



Kuna baadhi ya vitu vyangu viko kwake kitanda, godoro, sofa, DSTV, kapeti, jiko la gesi, mtungi vitu hivyo apewe kaka yangu Dickson wa Bariadi. Samahani kwa wazazi wangu, marafiki zangu kwa kitendo hiki naomba barua hii isomwe mbele ya watu wakati wakiniaga.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad