Aunt Ezekiel "Ndoa na Iyobo no Labda Nimzalie Mtoto Mwingine"


Ni staa ambaye hivi sasa ana jina kubwa kupitia sanaa yake ya uigizaji wa filamu aliyoianza miaka 10 iliyopita.

NINAAMINI hata wewe unayesoma ukurasa huu muda huu umeshawahi kulisikia jina la Aunt Ezekel.

Ni staa ambaye hivi sasa ana jina kubwa kupitia sanaa yake ya uigizaji wa filamu aliyoianza miaka 10 iliyopita.

Kama ulikuwa hufahamu, basi Aunt ni mtoto wa marehemu kiungo mahiri wa zamani wa Simba na Yanga, Ezekel Grayson ‘Jujuman’.

Ni binti fulani matata pindi ukimchokoza. Mfupi wastani mwenye shepu ya uchokozi na rangi nyeusi yenye mng’ao (kama bado hajajichubua.) Macho makubwa na mashavu ya kumwagika.

Kuna lingine pia, Aunt ameshawahi kushiriki shindano la Miss Tanzania. Kwa kifupi ni staa huyu amepitia mambo mengi magumu katika safari yake ya maisha mpaka kufikia hapo alipo.

Ameshawahi kucheza baadhi ya filamu kama Mrembo Kikojozi, Miss Bongo, Yellow Banana, House Girl and House Boy, Nampenda mke Wangu, Usiku wa Maajabu na nyingine nyingi.

Staa huyu pia amewahi kuwa kwenye uhusiano mbalimbali na hata kufikia kufunga ndoa mara mbili.

Kwa sasa yuko kwenye uhusiano wa kimapenzi na dansa staa wa Bongo fleva Diamond, Moses Iyobo baada ya aliyekuwa mumewe, Sunday Demonte kutumikia kifungo kule Dubai.

Aunt na Iyobo wamebahatika kupata mtoto mmoja wa kike anayeitwa Cookie.

Leo Aunt amepiga stori na Mwanaspoti na kuzungumza safari nzima ya maisha yake.

Hivi karibu Aunt alitoa filamu yake mpya baada ya kimya cha muda mrefu. Filamu hiyo inaitwa, Mama akiwa amemshirikisha mwanaye, Cookie.

“Cookie amecheza kama mhusika msaidizi katika filamu hiyo. Ni filamu ambayo imenigharimu Sh 12 milioni hadi inakamilika. Unajua mama ni muhimu katika maisha ya ndio maana nimeamua kutoa filamu hiyo.

“Binafsi sioni kitu kingine baada ya Mungu ni mama ndio anayefuatia,” Aunt anafunguka.

“Picha za filamu hiyo zimepigwa maeneo ya Kisarawe (Mkoa wa Pwani) na huko ndiko marehemu baba yangu alipokulia na nimeamua kufanyia kazi huko,” anaongeza.

Mwanaspoti lilimuuliza Aunt kwa nini soko la filamu limeshuka?

“Matendo machafu. Wasanii wa filamu ni sehemu ya watu waliochangia kushuka kwa soko la filamu nchini. “Inabidi tuwe wakweli tu ,maana hali ya sasa haifichiki kuhusu filamu. Kipindi hiki filamu zimepoteza mvuto na watu wamekuwa wakizungumza mengi ila ninachokiona ni matendo yetu machafu yanachangia.

“Mbona wasanii kama kina King Majuto bado wanafanya vizuri? Skendo zinayumbisha soko la filamu na siyo kitu kingine,” Aunt anafunguka.

Msanii huyo anafafanua skendo zinazotajwa zaidi kuwatikisa wasanii wa kike wa filamu ni kutoka na waumume wa watu.

Pia, kuolewa na kuachika pamoja na kubadilisha mabwana mara kwa mara.

Kwa upande wa wanaume kiki za kijinga, ulevi pamoja na kubadilisha wanawake.

“Hakuna kingine zaidi ya kuachana na skendo hizo za kijinga.”

Aunt anaamini bado filamu zina uhai ila kwa sasa zimedorora tu kwani Watanzania wanapenda filamu zao kuliko za nje ambazo haziwahusu kijamii wala kiutamaduni na nyingi hadi zitafasiriwe.

Kama kuna kitu ambacho Aunt hakipendi kukizungumzia ni kuhusu uhusiano wake na wanaume waliopita.

Lakini kitu ambacho watu wengi hawakifahamu Aunt aliwahi kufunga ndoa mara mbili na kuachana na ndoa hizo.

“Mwaka 2007 nilifunga ndoa ya bomani na mfanyabiashara maarufu, Jack Pemba, nilianza kuishi na Jack kama mke na mume huku akinisaidia katika mambo yangu ya sanaa.

“Baadaye alinizuia kwani alikuwa hapendi nitoke nyumbani na baada ya muda nilipata ujauzito kitu kilichomfurahisha sana na kunizawadia vito vya dhahabu vyenye uzito wa kilo moja.

“Lakini kwa bahati mbaya ilipofika miezi saba nilijifungua mtoto akafariki dunia,” anasema kwa majonzi.

“Ndoa ilikuwa nzuri, nilikuwa napata kila kitu nilichokitaka na kutembelea magari ya kifahari lakini kitu amba cho nilikish ind wa ni vipigo vikali nilivyokuwa nikivipata.

“Nakumbuka kuna siku alinipiga kiasi ambacho mashuka meupe yalikuwa kama yamepakwa rangi nyekundu. Bibi yangu alikuja kunichukua na nikaondoka moja kwa moja.”

“Baada ya kuondoka kwa Jack, nilianza kupigana katika maisha na niliingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine.

“Nikarudi kucheza filamu ambapo huko jina langu lilizidi kukua siku hadi siku, hivyo nikawa naendesha maisha yangu, mpaka nilipokutana na Sunday Demonte aliyekuwa anaishi Dubai.”

Baada ya kuwa na uhusiano wa muda na Demonte hatimaye Aunt na mwanaume huyo wakafunga ndoa.

Aunt alifunga ndoa ya Kiislamu na Demonte, Novemba 2012, ambapo alibadili dini na kuitwa Rahma.

“Unajua kazi yangu kipindi hicho ilikuwa ni uigizaji hapa Tanzania na kazi hiyo ndio ilikuwa kila kitu katika maisha yangu.

“Sasa watu walikuwa wanajiuliza mume Dubai miye Tanz ania, lakini nilikuwa nafanya kazi zangu kwa kutengeneza filamu kama tatu, kisha naenda Dubai kukaa na Sunday hata hivyo tulikuja kuachana,” anaeleza.

Aunt anasema mume wake alitiwa nguvuni na polisi wa Dubai akikabiliwa na makosa kadhaa, likiwemo la kuishi bila ya kuwa na kibali na kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 mwaka 2014.

Lakini kwa sasa yuko uraiani tangu mwaka 2016 baada ya kuachiwa huru kwa msamaha maalumu unaotolewa kabla ya kuanza kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kila mwaka.

Aunt hataki kuingia kwa undani kuhusu ndoa yake hiyo kama alipewa talaka au la.

“Kila mmoja kwa sasa ana maisha yake. Miye nina yangu na Sunday ana yake full stop.”

KWANINI AMEDUMU NA IYOBO?

Mara nyingi uhusiano wa mastaa huwa unakuwa na drama nyingi sana na Aunt haikutarajiwa kama angeweza kuendesha maisha na Iyobo.

Awali, wengi walidai Aunt alikuwa akijificha tu kwa Iyobo lakini kulikuwa mwanaume mwingine aliyekuwa na uhusiano naye. Kadiri watu wanavyoamini kuwa uhusiano huo utakufa, Aunty na Iyobo kwa sasa wanakaribia kutimiza takribani miaka minne.

“Kikubwa ni kuzungumza na moyo wako. Je, umetua mahali sahihi? Unapata faraja unapokuwa hapo?

Mimi na Iyobo tunasikilizana na kuheshimiana na hatuleteani ustaa katika uhusiano wetu,” anasema Aunt.

Hata hivyo, staa huyo anasema katika mapenzi huwezi kuishi bila ya migongano kwani alishawahi kumfumania Iyobo na yeye alishawahi kubambwa na meseji kwenye simu yake ikionesha mtu alikuwa anampenda na yeye akampotezea.

ANA MPANGO WA KUOLEWA NA IYOBO?

“Mambo ya ndoa ni mwanaume ndiye anayeamua. Lakini pia kufunga ndoa ni makaratasi tu kikubwa ni jinsi gani unaishi na mwenzako na na maelewano kwa kiasi gani.

“Lakini kwenye suala la kuongeza mtoto niko tayari hata kesho,” anasema na kuachia tabasamu.

“Mara nyingi kazi zake ni za kusafiri na anakutana na watu mbalimbali, inasumbua sana mpaka kuna wakati huwa nahisi kutaka kushindwa.

“Lakini nikiangalia meseji anazotumiwa, nagundua wasichana wanampenda tu kwa sababu ni mtu fulani.”

“Unajua napenda sana mwanaume asiyekuwa na kero. asiyependa kuzungumza sana yaani kiufupi sipendi gubu,” anamaliza Aunty.

Aunt alizaliwa Dar es Salaam. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Bunge mwaka 1993 hadi 1998. Alimalizia darasa la saba katika Shule ya Msingi Chanzige iliyopo Kisarawe, mkoani Pwani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad