KLABU ya Azam, imepanga kwenda nchini Uganda kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Azam ambao ni mabingwa wa Kombe la Kagame walilolichukua Ijumaa iliyopita kwa kuifunga Simba mabao 2-1, imepanga kwenda nchini humo na kucheza mechi kadhaa za kirafiki kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Menaja wa Azam FC, Philip Alando, alisema awali walipanga kwenda nchini humo, lakini waliahirisha kutokana na muingiliano wa ratiba ya Kagame.
“Baada ya kumaliza michuano hii ya Kagame, tunatarajia kwenda Uganda kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.
“Siku yoyote kuanzia sasa tunaweza kwenda huko kwa sababu awali tulipanga kwenda, lakini ratiba ilibadilika kutokana na kuingiliana na michuano ya Kagame, hivyo tutaenda na nyota wetu wote waliopo kikosini wakiwemo wale wapya,” alisema Alando.
Azam FC inayonolewa na Mholanzi, Hans van Der Pluijm, imepania kufanya makubwa msimu ujao ambapo miongoni mwa nyota waliosajiliwa ni Wazimbabwe, Donald Ngoma na Tafadzwa Kutinyu pamoja na Mganda, Nicholas Wadada.