Balaa la Kubambikiziwa Watoto

WANAUME watapata taabu sana! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya balaa la wanawake kuwabambikia watoto wanaume wao kuzidi kutikisa na kuwaachia maumivu makubwa wahusika, Risasi Mchanganyiko linakupa habari kamili.



Matukio ya wanaume kubambikiwa watoto kila kukicha yamekuwa yakizidi huku wengine wakijikuta wakichukua maamuzi magumu ya hata kuua wake zao au kuachana nao.



MO MUSIC YAMKUTA

Mwanamama Emilianne Masoud ‘Bad Gal PG’ hivi karibuni aliibuka na kuweka wazi kwamba mwanamuziki wa Bongo Fleva, Moshi Katemi ‘Mo Music’ amemtelekeza mtoto aliyezaa naye na alianza kukataa tangu akiwa na ujauzito wa miezi mitano. “Nilikutana na Mo Music baada ya kutaka kumsimamia kazi zake kama meneja wake kupitia kwa mpenzi niliyekuwa naye kwa wakati huo lakini tukagombana hivyo sikuweza kumsimamia tena kazi zake.



“Baada ya hapo tulianzisha uhusiano wa kimapenzi na Mo Music ambapo nilipata ujauzito nikamwambia akasema haina shida, ujauzito ukiwa na mwezi mmoja nilisafiri kikazi India maana nafanya biashara nikakaa miezi mitatu nikarudi hapo mimba ikawa ina miezi minne.

“Niliporudi Mo Music akataka nimpe laki tatu akalipie kodi ya nyumba nikamwambia sina hapo ndipo mgogoro ukaanza akasema kama ni hivyo basi hanitaki tena na mimba siyo yake, tukaachana.



AMPA MTOTO BABA MWINGINE

“Kutokana na kwamba Mo Music nilimuomba majina yake kamili ili niandike kwenye kadi ya mtoto ya kliniki akanikatalia, nilipojifungua nilimpa mtoto jina la baba mwingine ambaye alikuwa mpenzi wangu zamani kabla ya Mo Music kwani naye alijua mtoto ni wake lakini uhakika baba wa mtoto ni Mo Music.



“Niko tayari kupima DNA na Mo Music maana nina uhakika yeye ndiye baba wa mtoto wangu lakini amekuwa akimkana kwamba siyo wake, wakati hata kufanana wanafanana mno hata ndugu zake wanajua, ninachohitaji ni yeye kutambua kwamba ana mtoto tu na kumpa malezi na siyo kitu kingine,” alisema Emilianne.



MO MUSIC ANASEMAJE?

Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, Mo Music alisema hana mtoto bali ndiyo anategemea kupata kwa mpenzi aliyenaye kwa sasa, kuhusu huyo mwanamke hayuko tayari kupima DNA kwa kuwa ana wasiwasi mtoto siyo wake.



“Nina shaka sana na huyo mtoto siyo wangu maana huyo mwanamke alikuwa akijiuza India pia alikuwa na mwanaume wake mwingine, kingine ni kwamba kadi ya mtoto haijaandikwa jina langu, sasa mimi siwezi wala haiwezekani kukubali kwamba mtoto ni wangu, kwanza ananichafulia jina akicheza nitamshtaki,” alisema Mo Music.


MWINGINE ANYANG’ANYWA MTOTO

Katika tukio lingine, Aloyce Agostino ambaye ni mkazi wa Majumba Sita, Kisarawe mkoani Pwani amejikuta katika wakati mgumu baada ya kunyang’anywa mtoto ukweni kwani alikuwa akiishi na mpenzi wake aliyejulikana kwa jina la Hajrati Hamidu ambaye tayari alikuwa ameshamtolea barua ya uchumba ambapo waliishi kinyumba tangu mwezi wa sita mwaka jana.



Aliendelea kueleza kuwa walifanikiwa kupata mtoto wa kike ambaye ana miezi nane kwa sasa ambapo Mei, mwaka huu figisu zilianza kuibuka na mzazi mwenzake huyo kwani alimdanganya kwamba anakwenda kufanyia usafi makaburi ya wazazi wake lakini kumbe alikwenda kwa mwanaume mwingine. “Baada ya mzazi mwenzangu kusema kwamba anakwenda kufanyia usafi makaburi ya wazazi wake niliwasiliana na dada yake akasema hayupo huku, nikampigia simu yeye mwenyewe lakini alikuwa ‘ameniblock’.



“Siku tatu baadaye alirudi na alipofika akawa bize na simu kuna namba ikawa inampigia kila saa nikapokea ndipo akaongea mwanaume na kusema nimwache mwanamke wake na mtoto ni wake, nilishindwa kuongea naye ikabidi nikimbilie kwa dada yangu ndiyo akaendelea kuzungumza naye.

“Yule mwanaume akaeleza kwamba mtoto ni wake na alikuwa akimhudumia tangu huyo mzazi mwenzangu akiwa na ujauzito, baada ya hapo tulimuuliza mzazi mwenzangu tukiwa na ndugu zangu na wake akasema mtoto ni wangu lakini baadaye kesi ilihamia serikali ya mtaa na ustawi wa jamii ambapo huko ndipo alipokiri kuwa mtoto siyo wangu ni wa mwanaume mwingine aliyemtaja kwa jina la Jafari. “Hapo alisema kwamba wakati anakutana na mimi alikuwa tayari ana mimba ya mwezi mmoja lakini hakuniweka wazi na wakati wa ujauzito alikuwa anatumiwa fedha na huyo mwanaume licha ya kwamba tulikuwa tunaishi pamoja.



“Kutokana na hilo mwanamke aliamua kurudi kwao na mtoto kwa kuwa anaogopa na sasa kesi inaendelea ustawi wa jamii ambapo mwanamke alikiri kwamba mtoto ni wa huyo Jafari na siyo wangu ila ninachohitaji kwa sasa na ninaomba nisaidiwe ni kupima DNA maana nina uhakika mtoto ni wangu,” alisema Aloyce.



MAMA MTOTO ANASEMAJE?

Akizungumza Hajrati alisema kwamba mtoto huyo siyo wa Aloyce kwani wakati anaanza kuishi naye kinyumba alikuwa na ujauzito wa mwanaume mwingine, Jafari lakini baadaye alimwambia Aloyce ana ujauzito wake ndipo akamhudumia mpaka akajifungua.



“Wakati nakutana na Aloyce nilikuwa na ujauzito wa mwezi mmoja lakini sikumwambia bali nilipoishi naye kwa muda mfupi kama mwezi nikamwambia nina mimba maana huyo Jafari alikuwa safarini kwa wakati huo akawa ananitumia hela kwenye simu. “Sasa mwezi wa tano mwaka huu nilikutana na Jafari akamtaka mtoto wake ndipo ukweli ukajulikana hapo na sasa kesi ikimalizika nitaenda kuishi na huyo baba mtoto wangu maana hata kadi la mtoto nimeandika jina lake huyo Jafari na siyo Aloyce,” alisema Hajrati.

AWASHAURI WANAUME

Kutokana na kitendo hicho, Hajrati aliwashauri wanaume kuwa makini sana hasa pale wake au wapenzi wao wanawaambia wana ujauzito kwani wanawake wengi ni wadanganyifu mno.

NDUGU, MAJIRANI WAPIGWA BUTWAA



Katika mtaa huo wakazi wengi ambao ni ndugu na majirani waliozungumza na gazeti hili walijikuta wakipigwa butwaa kwa kitendo alichofanya Hajrati kwani siyo cha kawaida na hakijawahi kutokea hiyo ndiyo mara ya kwanza.

“Kiukweli tumeumia sana maana sisi tulikuwa tunampenda sana wifi yetu, tunamhudumia kwa kuwa tulijua kwamba mtoto ni wetu lakini kumbe alitufanyia ukatili wa aina hii, tunaomba tu DNA ihusike hapa ili tuujue ukweli kwani inawezekana anadanganya pia,” alisema Zawadi ambaye ni dada wa Aloyce.



TAKWIMU ZINASEMAJE?

Mwaka 2013, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali nchini ilieleza kuwa, karibu nusu ya watu waliojitokeza kupima vinasaba (DNA) ili kubaini uhalali wa watoto wao, vipimo vilionesha si wazazi halisi wa watoto waliopimwa. Takwimu hizo ni kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2010, ikionesha kuwa, asilimia 48.32 ya wazazi ‘wanalea’ watoto wasio wa kwao wakati asilimia 51.68 ndiyo wazazi halali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad