Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama ameeleza kufurahishwa na vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Hayo yameelezwa jana Jumapili Julai 15, 2018 na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga katika mkutano wake wa naandishi wa habari.
Dk mahiga alikuwa akieleza kwa ufupi mazungumzo yake ya Obama ambaye alitembelea hifadhi hiyo alipokuwa nchini.
“Obama amevutiwa na hifadhi ya Serengeti, ameahidi kuisaidia Tanzania kuvutia wawekezaji zaidi katika hifadhi hii. Amesema ameona mambo mengi ambayo hajawahi kuona akiwa na familia yake,” alisema Dk Mahiga.
Kuhusu usiri wa ujio wa Obama nchini, Balozi Mahiga amesema kiongozi huyo mstaafu alikuwa na ziara binafsi.
“Alikuja kutembelea hifadhi ya Serengeti ikiwa ni safari yake binafsi hivyo ni lazima tuheshimu,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema ujio wa Obama na familia yake umeitangaza Tanzania na kuungwa mkono na meneja uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete ambaye alisema ujio wa rais huyo mstaafu unatokana na jitihada za nchi kutangaza vivutio vya utalii.