Biti Zito la Kangi Lugola "Mimi ni Ninja, Ole Wenu Mnaotaka Kuharibu Amani Ya Nchi"


Waziri  wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema hatamwonea aibu kiongozi au mtu yeyote atakayetaka kuhatarisha amani ya nchi. 


Kutokana na hali hiyo, amesema kuanzia sasa, wanaotaka kuhatarisha amani, wajue kwa sasa ameuvaa uninja usoni.


Waziri Kangi aliyasema hayo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na viongozi wa taasisi, mashirika, mamlaka na taasisi za Serikali pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkoa wa Mbeya.


Katika maelezo yake, waziri huyo aliwataka viongozi wajiandae kwa uamuzi mgumu atakaoutoa baada ya kupokea taarifa kutoka kwenye mamalaka husika zinazojihusisha na usalama barabarani.


“Nilipokuwa bungeni, kuna baadhi ya watu walionekana kutaka kuharibu amani na mimi kulazimika kuvaa kofia ya kininja ambayo ilikuwa ya kitambaa.


“Lakini, kwa sasa nitalazimika kuvaa kofia hiyo ya chuma na nzito zaidi kwani ninaopambana nao ni makamanda wenzangu.


“Niliapishwa Jumatatu wiki hii kushika nafasi hii inayoyahusisha majeshi ya magereza, uokoaji,  idara ya uhamiaji, vitambulisho vya Taifa, wakimbizi, usajili wa vyama vya kijamii, makanisa na misikiti.


“Kwa kawaida, vyombo vyote hivyo ndivyo vinavyohakikisha amani ya nchi inakuwepo.


“Hivyo basi, wananchi wanapopata ajali mahali popote ikiwamo Mbeya na maeneo mengine ya nchi na wakati huo huo Serikali ikashindwa kuchukua hatua, basi nchi haitakuwa na amani wala utulivu.


“Kwa hiyo, sitanii bali nimeamua kuuvaa uninja nikimaanisha na sitamwonea haya mtu yeyote."
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad