Wakati ukiwa umesalia mwezi mmoja pekee huu wa saba kuelekea msimu mpya wa Ligi kuu Bara 2018/19, Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, ametoa masharti kadhaa kwa klabu zinazosajili wachezaji wa kigeni.
Kwa mujibu wa Radio One, Wambura amesema kwa kila timu inayotaka kusajili mchezaji wa kigeni ni lazima ihakikishe ana ubora wa kutosha na si ilimradi awe anatoka nje ya Tanzania.
Mbali na ubora, Wambura ameeleza mchezaji yoyote wa kigeni anapaswa kucheza na si kukaa benchi ili kuonesha kweli kuwa yeye ni wa kimataifa halisi na si wale ambao wamekuwa wakiletwa kisha wanashindwa kucheza.
Vilevile Wambura amezitaka klabu zote endapo zinasajili wachezaji wa kigeni ziwe na uwezo wa kuwalipa mishahara yao vilivyo na isije ikatokea wanadai kwa maana watachukua hatua kwa wahusika.
"Tunataka klabu ikishasajili mchezaji wa kigeni ni lazima kwanza iwe na uwezo wa kumlipa stahiki zake zote ikiwemo mshahara, hatutaki kusika anadai, pia tunataka mchezaji huyo awe na uwezo unaoashiria kuwa ni wa kimataifa na si wa kukaa benchi" alisema Wambura.