CCM Walaani, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Kumnasa Vibao Ofisa Ardhi
0
July 26, 2018
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Mjini kimelaani kitendo cha Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kumpiga vibao mtumishi wa ofisi yake, Damas Mwakindingo ndani ya ofisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Julai 25, 2018, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Robert Mwinje alisema kitendo alichokifanya Kunambi hakikubaliki kwa kuwa hakuna sheria inayoruhusu mtumishi kupigwa.
“Sisi kama Chama, kazi yetu ni kushauri lakini pia kushauri kuna mwisho wake,” alisema Mwinje.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mwinje alimbatana na madiwani wa CCM wa Jiji la Dodoma.
Hata hivyo, baadaye alipohojiwa kuhusu tuhuma hizo, Kunambi alisema hawezi kuongea chochote kuhusuiana na tuhuma hizo na badala yake akamtaka anayedai kupigwa ndiyo azungumza na waandishi wa habari.
“Mimi sina cha kuongea na badala yake ongeeni na huyo wanayesema nimempiga, ila mie nitakutana na huyo mwenyekiti (Mwinje) mahakamani,” alisema Kunambi.
Damas Mwakindingo ambaye ni ofisa ardhi wa Jiji anayedaiwa kupigwa na Mkurugenzi wa Jiji alikanusha vikali tuhuma hizo na kusema hajapigwa na Mkurugenzi wa Jiji.
“Ni watu tu wamezusha, kwani hata hivyo tulikaa na tukayamaliza, hivyo yamekwisha,” alisema Mwakindingo
Tags