CHADEMA yaipigia goti Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia Katibu Mkuu wake Dkt. Vicent Mashinji wameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kusimamia haki katika uchaguzi mdogo wa Ubunge na udiwani ambao umepangwa kufanyika Agosti 12 mwaka huu kwa kata 77 za Tanzania Bara.


Dkt. Mashinji ametoa Kauli hiyo leo Julai 12, 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam na kuitaka Tume hiyo kuendesha uchaguzi uliokuwa huru ili mradi amani na utulivu iendelee kuwepo nchini.


"Katika uchaguzi huu wa marudio kumeanza kujitokeza vitendo vya ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi, ikiwemo kughushi saini za viongozi ili kuhalalisha wagombea katika Halmashauri ya Tunduma mkoani Songwe kupitishwa kinyume na sheria. Tunaviomba vyombo vya dola kuwachukulia hatua wote waliohusika. Kutokuwa na uchaguzi huru kunaweza kusababisha machafuko katika nchi", amesema Dkt. Mashinji.


Pamoja na hayo, Dkt. Mashinji ameendelea kwa kusema "tunahitaji kuwepo na Tume huru ya uchaguzi na katika uchaguzi huu, Tume isimamie haki na hizi figisu figisu zilizoanza kujitokeza izimalize mapema pamoja na matukio ya wagombea kukamatwa na kunyang'anywa fomu zao za ushiriki".


Uchaguzi huo mdogo wa marudio umekuja baada ya kuwepo wazi Jimbo la Buyungu Mkoani Kigoma kufuatia Mbunge Kasuku Bilago kufariki dunia mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu pamoja na madiwani wa maeneo mbalimbali kuyaacha majimbo yao na kujiunga CCM kwa lengo la kumuunga mkono Rais Magufuli.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad