Chelsea imeanza mkakati wa kumshawishi kipa wake wa zamani Petr Cech kurejea Stamford Bridge.
Taarifa za Chelsea kutaka saini ya Cech zimekuja muda mfupi baada ya Arsenal kufungua milango kwa kipa huyo.
Kocha mpya wa Chelsea, Maurizio Sarri, amegoma kumpigia magoti kipa Thibaut Courtois anayetaka kujiunga na Real Madrid katika usajili wa majira ya kiangazi.
Sarri ameweka mezani majina ya makipa watatu akiwemo Cech, aliyecheza mechi 333 Chelsea kurejea katika klabu hiyo.
Makipa wengine wanaotupiwa jicho na Sarri ni kipa wa Leicester City Kasper Schmeichel na chipukizi wa AC Milan, Gianluigi Donnarumma mwenye miaka 19.
Sarri anaamini Cech atakuwa radhi kurejea Chelsea baada ya kocha mpya wa Arsenal, Unai Emery kumponda siku chache baada ya kutia saini mkataba wa kuifundisha timu hiyo na tayari amemsajili kipa wa Bayer Leverkusen ya Ujerumani, Bernd Leno mwenye miaka 26.
Sarri ametua Chelsea kujaza nafasi ya Mtaliano Antonio Conte aliyetupiwa virago baada ya kushindwa kuipa mafanikio katika mashindano ya Ligi Kuu England msimu uliopita. Licha ya kuipa ubingwa Chelsea katika msimu weke wa kwanza, Conte aliibua mzozo baada ya kumtimua Diego Costa.