China inavyoitikisa Marekani kiuwekez


Haya ni baadhi ya masuala ya uwekezaji yanayoonyesha kuwa China taifa linaloibukia kuwa na nguvu zaidi duniani linainyemelea, kuinunua na kuimaliza  Marekani kiuchumi, kama ilivyoandikwa kwenye mtandao wa Industry Week.

“Sisi Waamerika kwa muda mrefu tunapuuza athari zinazotokana na  kuruhusu kampuni na mashirika ya kigeni kununua mali zetu ziwe kampuni, ardhi na maliasili nyingine.Tunauza uwezo wetu wa kuzalisha mali na utajiri kwa wageni kwa kuruhusu mashirika yetu mengi kununuliwa na wageni.Lakini si wageni tu ni mashirika ya Kichina , tena kampuni zinazomilikiwa na Serikali ya China .Ni hatari kwani China inatumia mashirika yake ya umma kimkakati kwa kujifanya kuwa ni kampuni binafsi zinazoendeshwa kwa nguvu ya ushindani wa soko na imetungiza mkenge na kutufanya tuonekane kama majuha wakubwa wanaodanganyika kwa wepesi hapa duniani.” Inasema taarifa ndani ya mtandao wa  ‘Industry Week’  kwenye makala iliyoandikwa Januari 2018.

Hivi ni nani aliyeguswa na taarifa za kuuzwa kwa kiwanda kikubwa cha kuzalisha bidhaa za nguruwe cha Marekani cha ‘Smithfield Foods,’kununuliwa na shirika moja la China mwaka 2013?

Wanahisa waliruhusu mauzo kwa mwekezaji kampuni ya Shuanghui International Holdings Limited, mwekezaji mkubwa na msindikaji wa nyama wa China.

Ni wachache waliotafakari wakati kampuni ya Hoover, ilipouzwa kwa kampuni ya kielektroniki ya Hong Kong, iliyoko China iitwayo Techtronic Industries, muamala uliofanyika mwaka 2006 , baada ya kampuni ya Maytag, iliyokuwa inamilika Hoover, iliponununuliwa na Whirlpool.

Hoover ni kampuni iliyokuwa inazalisha vifaa vya usafi vya kielektroniki. Mashine za kusafisha vitu mbalimbali kwa kutumia ‘presha’ yanayotumiwa kusafisha mazulia, viyoyozi, injini za magari na kompyuta,wakati Whirlpool ni kampuni ya kuzalisha vifaa vya jikoni kama majiko, friji na mashine za kuoshea vyombo.

Aidha, Januari mwaka 2014, ulianza kwa kampuni ya Motorola Mobility kuuzwa kwa kampuni ya kielektroniki na teknolojia za kompyuta ya Kichina ya Lenovo yenye makao makuu jijini Beijing.

“Hii inamaanisha kuwa taifa kubwa lililogundua utaalamu na uwekezaji wa simu za mkononi ambalo ni Marekani limetupwa nje ya ulingo wa kuzalisha simu hizi. Muamala huu na mauziano umeipa China, teknolojia babu kubwa na uwezo wa juu wa kuzalisha simu duniani. Lenovo hiyo ndiyo tena iliyoinunua kampuni ya kompyuta ya IBM’mwaka 2004.” Inalalamika makala ya Industry Week.

“Kwa kutumia mkakati huo wa serikali kufanya manunuzi ya kampuni zetu, China imejiwezesha kuwa taifa linalotuuzia vifaa na mahitaji yote ya kinishati . Kuanzia 2009, kampuni zake zimewekeza mabilioni ya dola kununua hisa za kampuni za nishati kama The AES Corp., Chesapeake Energy, Oil & Gas Assets. Katika mwaka wa 2010, Kampuni ya Mawasiliano ya Kichina ya China Communications Construction Co. ilinunua asilimia 100 ya kampuni ya Friede Goldman United, wakati mwaka 2012, kampuni ya nguvu za upepo ya A-Tech Wind Power (Jiangxi) ilinunua kwa asilimia 100 kampuni ya Cirrus Wind Energy.”

Mwaka 2016, hoteli  bora za Marekani za Starwood Hotels , zilinunuliwa na Anbang Insurance, kampuni ya bima ya Kichina, ambayo sasa imecharuka kununua hoteli za Marekani. Mwaka jana kampuni hiyo ya bima ilinunua hoteli ya kisasa iliyoko New York ya Waldorf-Astoria. Hoteli ya Starwood ikaongeza idadi ya hoteli zilizonunuliwa na China kufikia 1,300 kote duniani mmiliki akiwa ni kampuni hiyo ya Beijing ya Anbang.

Kampuni nyingine ya Marekani ambayo sasa iko mikononi mwa Beijing ni Ingram Micro, ilinunuwa na Tianjin Tianhai Investment Development Company, inayojihusisha na usafirishaji wa anga na vifaa vya aina na matumizi mbalimbali.

Nyingine ni General Electric Appliance Business, iliyonunuliwa na Qingdao Haier Co, wakati Terex Corp yenye miaka 83, iliyokuwa na makao yake makuu jijini Connecticut, ikizalisha mashine na vifaa vya ujenzi, kilimo na viwanda ilipigwa mnada na kununuliwa na  Zoomlion Heavy Industry Science ya Beijing.

China inanunua hadi masuala ya burudani inaelezwa kuwa imenunua kampuni ya Legendary Entertainment Group, ambayo awali ilikuwa ikishirikiana na wadau kudhamini na kufanikisha sinema kali duniani kama Jurassic Park, Godzilla na Pacific Rim, sasa ziko mikononi mwa Wachina ndani ya kampuni yao ya Dalian Wanda.

Dalian Wanda, ilinunua pia kampuni ya burudani ya AMC Entertainment Holdings, iliyokuwa kampuni ya pili kwa ukubwa ya Marekani ya kutengeneza sinema wakati inauzwa, leo imepanda ni ya kwanza kwa ubora.

CHANZO

“Nchi nyingi haziruhusu umiliki wa asilimia 100 wa kampuni zake kwa wageni , lakini Marekani haibabaiki. Tunaruhusu kampuni za Kiamerika kuuzwa kwa wageni , labda kwa zile ambazo zina masuala ya usalama na maslahi ya taifa. Lakini cha kushangaza hatuoni mataifa tunayoyauzia yakituuzia kampuni zake.

Serikali ya China inadhibiti na kuzuia kampuni za kigeni kumiliki viwanda vyake kwa asilimia 100. Inasisitiza ubia kwa kampuni na viwanda vyake kwa kila anayetaka kuwekeza.

Kinachowawezesha Wachina kununua mali zetu ni pengo kubwa la kibiashara baina yetu na China. Ndiyo maana wanajichukulia kidezo makampuni yetu kwa vile kila tunapouza bidhaa hatuwatoshelezi na wanahitaji zaidi, wakati sisi tunanunua kidogo kutoka kwao.

Kwa takribani miaka 20 sasa tumekuwa tukiuhamishia utajiri wa Amerika kwa Wachina tukiwatajirisha kwa mamilioni ya dola. Mwaka 1994,pengo la kibiashara  (trade deficit) kati ya Marekani na China lilikuwa dola bilioni 29.5 , na lilikua hadi kufikia dola bilioni 83.8 mwaka 2001 wakati China ikipewa makaribisho makubwa kwenye Shirika la Biashara Duniani (WTO) ikiheshimika kama taifa linalokubalika zaidi duniani.

Kwa miaka mingi pengo hilo limekua na kuongezeka na sasa ilipofika 2016 limefikia dola bilioni 347.

KUTOTUMIA SHERIA

Kwa nadharia Marekani ina uwezo wa kuzuia uuzwaji wa mashirika yake kupitia kamati ya kuishughulikia  uwekezaji wa kigeni ‘Committee on Foreign Investment in the United States- CFIUS.’

Kamati hii ina mamlaka kisheria kurekebisha, kukataa au kuidhinisha ununuzi wa mashirika na uwekezaji wowote wenye mashaka, lakini CFIUS haijatumika kudhibiti ununuzi huu.

Athari za kampuni za kigeni kununua mashirika ya Marekani zilitajwa na mwaka 2013 na Ripoti ya Baraza la Bunge la Juu (Congress) ya Mapitio ya Kiusalama katika uwekezaji baina ya China na marekani.

Ilionya kuwa:“China inawasilisha kitisho kipya kwa kamati ya CFIUS, kwa sababu uwekezaji unaofanywa na mashirika yake ya umma unaweza kuondoa ama kutatiza mipaka baina ya usalama wa taifa na wa uchumi na uwekezaji .”

China inatajwa kuwa ina kiasi kikubwa cha akiba ya fedha za kigeni kwenye benki kuu kikifikia dola trilioni  3.66 na inahofiwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ni dola. Aidha ina mabilioni ya mali (assets) yaliyo kwenye ardhi,majengo, utaalamu na teknolojia vyote hivyo vikitikisa mahasimu wake.

Tanzania na Afrika zinaweza pia kujifunza kile kinachotokea miongoni mwa mataifa haya makubwa na kujipanga vizuri kwenye uwekezaji wa miradi ya kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad