KUFUATIA kusambaa kwa picha zikimuonesha akiwa ametinga kikuku mguuni kisha kushambuliwa akihusishwa na skendo ya ushoga, hatimaye staa wa Afro-Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amevunja ukimya.
Mara baada ya picha hizo kusambaa na kuibua gumzo huku baadhi ya watu wakimtolea povu, Diamond alianza kuitwa shoga, skendo ambayo ilikamata vilivyo hasa kwenye mitandao ya kijamii na kumjengea picha tofauti kwa mashabiki wake.
MASHABIKI WAKASIRISHWA
Baadhi ya mashabiki hao kwenye mitandao hiyo walikasirishwa na kitendo hicho hivyo kummwagia matusi ya nguoni kutokana na kuchukizwa na kitendo hicho. Hoja kuu kutoka kwa mashabiki hao ilikuwa kwamba, jambo hilo haliendani na utamaduni wa Kitanzania na kwamba wanaofanya hivyo ni mashoga na lengo lake ni kuharibu vijaja wadogo wa Kitanzania.
DIAMOND HAKUPEWA NAFASI
Katika hali kama hiyo, Diamond hakupewa nafasi ya kujitetea au kufafanua juu ya jambo hilo hivyo Ijumaa Wikienda lilijipa jukumu la kumtafuta ambapo alifichua siri ya kutinga kikuku hicho.
MAHOJIANO AKIWA MAREKANI
Katika mahojiano na gazeti hili akiwa kwenye ziara ya kimuziki nchini Marekani, awali Diamond alikuwa mkali akionesha kuchukizwa na jambo hilo alilodai ni baya mno na kwamba hata yeye anachukizwa na vitendo hivyo vichafu. “Kwanza sijui kama kile ni kikuku, nilivaa kama ninavyovaa mikufu au cheni.“Niliona ni urembo kama urembo mwingine na kwamba haiwezi kuwa ishu kubwa kama ilivyotokea,” alisema Diamond.
Aliendelea kutirika kuwa, ni vyema ikafahamika kwamba, hata yeye anachukizwa sana na tabia ya ushoga kwa hiyo aliwataka wanamwita shoga kuacha mara moja. “Ninawaomba chondechonde waache kunihusisha na jambo hilo baya, ujue nyuma yangu kuna watu wengi mno wanatamani kuwa kama mimi hasa vijana wadogo.
“Sasa wakiona ninahusishwa na jambo ambalo linapigwa vita nchini mwetu, wataacha kunifuatilia kama mtu wanayetamani kuwa kama yeye,” alisema Diamond na kuongeza: “Lakini unajua imekuwa ni kasumba kwa watu maarufu kuhusishwa na jambo hilo ili kuwajengea picha fulani kwa mashabiki au wafuatiliaji wake.
AMTAJA MICHAEL JACKSON, RONALDO
“Mtu kama marehemu Michael Jackson (aliyekuwa staa wa Muziki wa Pop duniani) alikuwa akihusishwa na ushoga, lakini hakuna aliyekuwa na ushahidi labda ilitokana tu na ishu za kujibadilisha mwili au sura. “Kwa hiyo si jambo geni kwa watu maarufu kusikia eti fulani ni shoga. Jambo hilo linaweza kuwa linatengenezwa na mpinzani wako.
“Hata Cristiano Ronaldo (mchezaji wa Timu ya Juventus ya Italia aliyetua akitokea Real Madrid) amekuwa akihusishwa na ushoga, lakini amekuwa akipotezea na kuendelea kupiga hela. Kama nilivyosema si jambo geni lakini limenichefua sana.
AOMBA RADHI
“Najua mimi kama mtu wao nimewaudhi hivyo ninawaomba radhi na nisingependa waendee kunihusisha na dhambi hiyo.”
STORI: GPL