MUZIKI bwana! Miaka ya 2000 katikati waliibuka wasanii wengi wadogo kiumri, walikuwa na uwezo katika kuimba na kurap lakini kutokana na udogo wao, majina yao wakaamua yasiwe mbali na umri wao.
Mfano aliibuka Aslay Isihaka na Wimbo Naenda Kusema, kutokana na udogo wake akaamua kujiita Dogo Aslay lakini kadiri alivyokuwa kiumri jina la dogo limepotea na sasa anatambulika kama Aslay.
Akaja David Genzi ‘Young Dee’ na Ngoma ya Tunapeta, akapeta kweli, leo hii umri umeenda si dogo tena, kaamua kulitema taratibu jina la Young Dee na sasa anataka kutambulika kama Paka Rapa.
Ukija kwa Eric Msodoki ‘Young Killer’ naye alianza na Ngoma ya Dear Gambe, alikuwa kweli mdogo kiumri lakini uwezo wa kurap ulikuwa juu, umri ulivyoanza kwenda na kuwa kijana akaamua kulizima taratibu jina la Young Killer na kujiita Msodoki.
Tukija kwa msanii kutoka Manzese Music Baby (MMB), Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’ jina lake hilo lilikuwa miongoni mwa madogo waliokuwa wakisumbua kwenye gemu la Hip Hop Bongo. Baada ya kuona umri naye umeanza kusogea taratibu alianza kuchenji jina na kutambulika kama Janjaro.
Image result for dogo janja
Janjaro ni mmoja kati ya wanamuziki naweza kusema ameweza kukaa kwenye gemu la Muziki wa Hip Hop Bongo tangu mdogo. Ukisikiliza Ngoma ya Anajua aliotoka nayo kimuziki akimshirikisha Tunda Man kisha Nisikilize akiwa na Madee halafu ukaja ukalinganisha na ngoma zake za miaka ya hivi karibuni kama vile My Life, Kidebe, Ukivaaje Unapendeza na Ngarenaro utaelewa namaanisha nini.
Kwa sasa Janjaro ameachia kichupa kipya kinachoitwa Banana ambapo ukikiona na kusikiliza staili aliyoitumia katika kufikisha ujumbe utagundua ‘dogo’ kakua. Haya hapa mahojiano yake kwa ufupi juu ya ngoma hiyo;
Star Showbiz: Kwanza hongera kwa kazi yako, kwa nini umeamua kuitambulisha nje ya nchi kabla ya nyumbani?
Janjaro: Asante, kwanza nilikuwa nataka kufanya kitu cha kitofauti.
Star Showbiz: Unavyoona imeleta matokeo unayoyataka?
Janjaro: Imekuwa kubwa kwa sababu imepitia vituo vikubwa vya muziki kama Trace Afrika na Trace Muziki.
Star Showbiz: Umekaa peke yako kwenye wimbo, hukutaka kuwa wa kitofauti?
Janjaro: Hapana kwa sababu nimemwimbia mke wangu.
Star Showbiz: Video yake umeifanya wapi labda?
Janjaro: Kichupa kimesimamiwa na Travellah wa Kwetu Studio na nimekifanyia nchini Afrika Kusini ‘Sauz’.
Star Showbiz: Kipya kipi mashabiki wako watarajie kwenye nyimbo zako?
Janjaro: Kikubwa nimebadilika, naimba staili tofauti kabisa zikiwa na mchanganyiko wa ragga f’lan na hata kwenye ngoma yangu hii ya Banana utaona utofauti.
Star Showbiz: Wimbo uliopita wa Mbayumbayu, mkeo (Uwoya) alishiriki kwa asilimia kubwa ikiwemo kukupamba na kukupa ‘dela’ lakini huu inaonekana kama hakuna sapoti kihivyo, tatizo nini?
Janjaro: Amesapoti na huwa anasapoti sana si ni mke wangu.
Star Showbiz: Labda tutegemee sapraiz ya kitu gani baada ya kuachia ngoma hii ya Banana?
Janjaro: Yeah! Kwa sasa natarajia kufanya World Tour yaani kutembelea nchi mbalimbali.
Star Showbiz: Msanii gani ungependa kufanya naye kazi ambaye hukuwahi kufanya naye?
Janjaro: Bongo bado sijajua wote wa kawaida ila kwa nje wapo wengi kama vile kina Elton John.
Star Showbiz: Mastaa wengi wanapofunga ndoa muziki kwao huwaendea kombo kwako imekaaje?
Janjaro: Kwangu ndoa imefanya muziki wangu kuwa muruaa, nina ndoa na muziki kama kawa ngoma zinatiririka tu!
Chanzo: Global Publishers
Dogo Janja Afunguka Kuhusu Ndoa Yake Ilivyosababisha Muziki Wake Kuwa Muruwaa
July 03, 2018
Tags