Donge kubwa la barafu lililopo katika maji limekaribia kijiji kimoja magharibi mwa Greenland na kusababisha uokoaji iwapo lingevunjika na mawimbi yake kusababisha mafuriko katika nyumba za kijiji hicho.
Barafu hiyo imepita nyumba hizo kwa urefu katika kijiji hicho na haikusongea siku moja ,kulingana na vyombo vya habari vya eneo hilko.
Maafisa wa eneo hilo wanasema hawajawahi kuona donge kubwa la barafu kiasi hicho.
Msimu wa jua uliopita , watu wanne walifariki baada ya mawimbi kusababisha mafuriko katika nyumba kadhaa kaskazini magharibi mwa eneo la Greenland kufuatia tetemeko la ardhi.
Wanakijiji 169 wanaoishi karibu na donge hilo la barafu wameokolewa kulingana na chombo cha habari cha Denmark Ritzau.
''Kuna nyufa na mashimo yanayotufanya kuwa na hofu kwamba huenda donge hilo likavunjika , mwanachama wa baraza la kijiji hicho Susanne Eliassen aliambia gazeti la eneo hilo la Sermitsiaq.
''Kampuni ya umeme na matangi ya mafuta ya kijiji hicho yapo karibu na ufukwe wa kijiji hicho'', alisema.
Baadhi ya wataalam wameonya kuhusu kutokea kwa madonge mengi ya barafu kutokana na mabadiliko ya hali ya anga, hatua inayozidisha hatari ya kutokea kwa vimbunga vya Tsunami.
Mnamo mwezi Juni wanasayansi wa chuo kikuu cha New York walitoa kanda ya video ya donge kubwa la barafu lililokuwa likivunjika mashariki mwa Greenland.