Kaka wa Mbunge wa Singida Mashariki, Alute Mughwai amesema wanatarajia kwenda mahakamani kudai haki ya kisheria ya matibabu ya ndugu yao Tundu Lissu aliyeshambuliwa na risasi Septemba 07, 2017.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Mughwai amesema wanachukua hatua hiyo baada ya Bunge kuiandikia barua familia hiyo, ikieeleza kuwa kuanzia sasa haitajishughulisha na matibabu ya mbunge huyo.
Mughwai amesema Juni 18, 2018 walipokea barua kutoka uongozi wa Bunge kuwa haitajishughulisha na matibabu ya mbunge huyo kwa kuwa yuko nje ya nchi kwa utaratibu binafsi na hakufuata utaratibu wa matibabu.
Mughwai amesema kutokana na hali hiyo wanaangalia utaratibu wa kwenda mahakamani kuangalia kama mwakilishi huyo anahaki kisheria ya kupatiwa matibabu ama la.
Kwa sasa Tundu Lissu yupo nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu amabyo kwa mujibu wake na familia pamoja na chama chake matibabu hayo yanalipiwa na wasamaria wema.