Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA), limeweka wazi mwamuzi atakayechezesha mchezo wa fainali ya kombe la dunia kati ya Ufaransa dhidi ya Croatia, itakayopigwa jumapili Julai 15 kwenye uwanja wa Luzhniki jijini Moscow Urusi.
Mwamuzi Néstor Fabián Pitana ambaye ni raia wa Argentina ndio amepewa nafasi ya kuamua mchezo huo wa fainali. FIFA imemteua Pitana baada ya kufanya vizuri katika mechi 4 alizochezesha kwenye fainali za mwaka huu, akianza na mechi ya ufunguzi Russia dhidi ya Saudi Arabia, Mexico dhidi ya Sweden katika hatua ya makundi, mechi ya 16 bora kati ya Croatia and Denmark pamoja na ile robo fainali ya Uruguay na France.
Hizi ni fainali za kombe la dunia za pili kwa Pitana kuchezesha akianza mwaka 2014 nchini Brazil na hiyo ilikuja baada ya kupata leseni ya FIFA mwaka 2010. Anauzoefu wa kuchezesha michuano mbalimbakli ya kimataifa ikiwemo Copa Amerika mwaka 2015.
Pitana mwenye umri wa miaka 43, amekuwa Muargentina wa pili kuchezesha mechi ya fainali ya kombe la dunia akitanguliwa na Horacio Elizondo ambaye alichezesha mechi ya fainali mwaka 2006 kati ya Ufaransa dhidi ya Italia ambapo Italia waliibuka mabingwa.
Pitana atasaidiwa na waamuzi Hernan Maidana, Juan P. Belatti wote wakitoka Argentina huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Bjorn Kuipers kutoka Uholanzi. Kabla ya kuanza rasmi kazi ya uamzi mwaka 2007, Pitana alikuwa muigizaji na mwalimu wa elimu ya viungo vya mwili.
Mwamuzi Alireza Faghani wa Iran yeye ameteuliwa kuchezesha mechi ya kutafuta mshindi wa 3 kati ya Ubelgiji dhidi ya England. Moja ya filamu ambazo pitana ameigiza ni pamoja na The Fury iliyotoka mwaka 1997 na Recopa Sudamericana iliyotoka mwaka 2005.