Giza latanda Chadema, Mgombea Atoweka


Giza la sintofahamu ladaiwa kutanda Mkoa wa Iringa, ikiwa ni baada ya mgombea wa udiwani kwa tiketi ya CHADEMA kutojulikana alipo baada ya kuchukuliwa na na watu wasiojulikana mapema ya leo.

Akizungumza na www.eatv.tv, kuhusu sintofahamu hiyo kwa njia ya simu, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema kwamba sintofahamu hiyo ilianza kujitokeza siku ya juzi baada ya aliyekuwa mgombea wa Kata ya Kwakilosa kunyang'anywa fomu na mtu aliyemuonyesha bastola hali iliyomuingiza woga mgombea Godfrey Luchagile na kumfanya ajitoe katika kinyang'anyiro hicho.

Akizidi kufafanua Msigwa amesema kwamba mgombea mwingine wa Kata ya Galilonga, Pallaiga Andrew yeye amekamatwa na jeshi la polisi kwa kosa la kugushi fomu ya uchaguzi akiwa eneo la kurudisha fomu yake.

"Hii ilianza juzi baada ya Mgombea Godfrey Luchagile, kudai kutishwa na bastola kisha kunyang'anywa fomu ya uchaguzi, baadaye mgombea aliyepatikana kuziba nafasi yake ndg. Hamid Mfalingungi naye kapotea mapema ya leo, huyu wa Galilonga yeye alinyang'anywa fomu lakini bahati nzuri alikuwa ameshaitoa 'photocopy' wakati anairudisha anaambiwa kagushi hivyo wamempeleka polisi ili kupoteza muda wa kupokea fopmu. Hatujui nia yao kwani katika Kata tatu tumemaliza zoezi hili salama ila hizi mbili ndiyo mambo haya yanaibuka,"

Akizungumzia kwa undani kuhusu tukio hilo, Katibu wa CHADEMA mkoani Iringa Jackson Mnyamwani amesema kuwa wakati sinema hiyo inaendelea Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, kata ya Kwakilosa, Ndg. Fuad Mwakitosa amegoma kupokea fomu ya mgombea ambaye ilirudishwa na wadhamini wake kitu ambacho ni kinyume na utaratibu.

Pamoja na hayo, Mch Peter Msigwa amesema kwamba tayari siku ya jana walikwisha wasiliana na Mkurugenzi wa Uchaguzi Taifa Athuman Kihamia kwa ajili ya sintofahamu hiyo lakini mpaka sasa hakuna kitu kinachoonekana kuendelea.

Hata hivyo www.eatv.tv, ilipomtafuta Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Juma Bwire kuzungumizia matukio hayo simu yake haikupokelewa, na juhudi za kumpata Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Ndg. Fuad Mwakitosa bado zinaendelea.

Uchaguzi wa marudio unatarajiwa kufanyika Agosti 12, 2018, katika jimbo la Buyungu, Kigoma na kata 77 baada ya madiwani wengi kuhama vyama vya upinzani na kuhamia CCM wakidai wanaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

UPDATE

Mgombea wa Udiwani Hamid Mfalingungi amepatikana akiwa kituo cha polisi, hajaruhiswa kuzungumza na mtu yoyote.

Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Iringa, Jackson Mnyamwani amethibitisha kuonekana kwa mgombea huyo ambapo amesema mgombea wao ameonekana muda mfupi baada ya muda wa kurejesha fomu za uchaguzi kuisha.

Amebainisha kwamba kwa sasa wanawasiliana na makao makuu ya chama ili waweze kupata msaada wa kisheria wa kujua jambo gani la kufanya kuweza kupata haki yao.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad