Rais John Pombe Magufuli amemtaka Msajili wa Hazina , Ndg. Athumani Mbuttuka kuhakikisha anatumia sheria aliyopewa na serikali pamoja na Bunge dhidi ya mashirika ambayo hayashiriki kwenye kujenga uchumi wa nchi haswa katika ulipaji kodi na utoaji wa gawio kwa serikali.
Rais Magufuli ametoa kuli hiyo mapema leo wakati akipokea gawio kutoka kwa Wakala, Kampuni Taasisi na Mashirika ya umma, kwa mwaka wa fedha 2017/2018, ambapo amemtaka Msajili kutazama kama atawafukuza viongozi wa mashirika, kuyafuta au kuwafilisi kulingana na sheria inavyomuongoza.
Rais Magufuli amesema katika uwekezaji uliofanywa na serikali wa zaidi ya shilingi trilioni 49, kisha kuja kupokea kiasi cha gawio kiasi cha bilioni 736 ni dogo sana kitu ambacho si sahihi.
Magufuli amesema uongozi wa mashirika hayo ubadilishwe au shirika lifutwe kwa kuwa hakuna haja ya kuwepo na mashirika jina ambapo ameongeza kwamba “ni nafuu usiwe nacho kuliko kuwa na kitu kichoshiriki kwenye kujenga uchumi”.
“Hakuna haja ya kukaa na mashirika ambayo yapo tu kwa jina. HAPA PESA KWANZA. Halipendwi shirika inapendwa pesa” amesema Rais Magufuli.
Wakati huo huo Rais ameyapongeza mashirika 47 yaliyoweza kutoa gawio jumla ya Bilioni 7 ambapo amewataka mashirika ambayo hayajatoa hata shilingi waanze kuona aibu.