Hatimaye watanzania kumiliki ardhi ghorofani


Serikali imeandaa mpango mji mpya katika jiji la Dar es Salaam utakaowezesha wananchi kupata hati miliki ya ardhi juu ya nyumba (ghorofani) na kuwa na haki sawa kama mmiliki wa kiwanja na katika mpango huo wananchi wenyewe ndiyo watakaopanga matumizi ya ardhi yao.


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Julai 27, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema lengo la mpango huo ni kuongeza upatikanaji wa maeneo kutokana na ongezeko la watu katika jiji hilo linalokadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni sita.

 “Aidha, licha ya kupangwa kwa matumizi mapya ya ardhi hakuna mwananchi atakayevunjiwa nyumba yake badala yake mtu yeyote atakayetaka kuendeleza maeneo ya wananchi atatakiwa kukubaliana nao na kuwalipa fidia ili wahame”, amesema Lukuvi.

Waziri Lukuvi ameongeza kuwa hatua ya mwisho ya uidhinishaji wa mpango mkuu wowote kwa mujibu wa sheria ya mipango miji ya mwaka 2007 inataka wadau wakutane waipitie, hivyo baada ya kuidhinishwa kwa mpango huo wataipeleka kwa wananchi kwenye kata mbalimbali na kwenye vikao vya madiwani kisha Waziri wa Ardhi ataitangaza.

Akimalizia, Lukuvi amesema wamefanya hivi kwa sababu Dar es Salaam ya sasa inaendelezwa bila utaratibu, kwahiyo wameandaa ‘master plan’ hii iwe dira ya upimaji na uendelezaji wa jiji la Dar es Salaam.

Endapo Tanzania itafanikiwa kupitisha mpango huo itakuwa imeungana na mataifa mengine kama Kenya, Tunisia na India ambayo tayari mpango huo umeshaanza kufanya kazi kutokana na ongezeko la watu katika maeneo hayo na kupelekea ufinyu wa ardhi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad