Hiki Hapa Chanzo cha Ajali Zinazotokea Mbeya

Hiki Hapa Chanzo cha Ajali Zinazotokea Mbeya
Ikiwa ni siku tatu tu, tangu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, kutangaza mabadiliko ndani ya jeshi la polisi nchini ili kuongeza juhudi za kuzuia ajali zilizotokea mara kwa mara katika baadhi ya Mikoa, jijini Mbeya bado hali ni tete kutokana na jiografia ya eneo hilo.

Siku chache tu tangu Jiji hilo lipoteze watu 20 na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mteremko wa Mbalizi Mkoani humo, ambapo ilikuwa pia ni siku chache tangu kutokea kwa ajali iliyosababisha vifo vya Askari wa Jkt, katika mteremko mkali wa eneo la Igodima na kufanya mpaka sasa kuwa na ajali tatu kubwa ndani ya kipindi cha miezi miwili, ukijumlisha na ajali iliyotokea usiku wa jana.

Watu wanne wamefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa katika  ajali ya barabarani iliyotokea Usiku wa jana jijini humo, iliyohusisha magari matatu tofauti yaliyogongwa na roli lililokuwa limefeli breki katika mlima wa Igawilo jijini humo.

Kwa mujibu wa Kaimu RPC Mkoa wa Mbeya, Mussa Taibu amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo mkali wa dereva ambaye alikuwa amebeba mzigo mzito kwenye kontena na kupelekea kufeli kwa breki.

“Ajali hiyo imehusisha magari matatu imetokea kwenye mteremko wa mlima Igawilo gari lenye kontena limeliangukia gari aina ya Noah iliyokuwa na abiria na inasadikiwa watu wanne wamepoteza maisha bado zoezi la uokoaji linaendelea kwani jana usiku tulishindwa kuondoa kontena kwakuwa uzito ulikuwa umezidi”, amesema Kaimu Kamanda.

Akizungumzia jiografia ya eneo hilo Kamanda Taibu amewataka madereva na watumiaji wa barabara kuwa makini, na kufanya ukaguzi wa magari yao kabla ya kuanza safari kwani ajali nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva kuendesha magari mabovu.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad