Hiki ndicho Alichoamua Hakimu baada Mbowe na Mashinji kutofika Mahakamani


Viongozi 9 wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi ya kufanya maandamano isivyo halali akiwemo Freeman Mbowe wanatarajiwa kusomewa maelezo ya awali (Ph), July 31,2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. 

Hatua hiyo imefikiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi kuomba wapangiwe tarehe ili washtakiwa wasomewe maelezo ya awali. 

Nchimbi amedai kuwa hatua hiyo inakuja kwa sababu July 20, 2018 Mahakama Kuu ilitupilia mbali maombi ya marejeo ya Mbowe na wenzake kuhusu maamuzi yanayotolewa na Mahakama ya Kisutu. 

Hata hivyo, Wakili wa utetezi Nashon Nkungu kwa niaba ya Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya amedai kuwa ni kweli Mahakama Kuu iliyatupilia mbali maombi yao ya marejeo lakini walionesha nia ya kukata rufaa na wamekwisha peleka kusudio la kukata rufaa Mahakama Kuu siku hiyo hiyo. 

Kutokana na hoja za kisheria, Hakimu Mashauri amesema anaahirisha kesi hadi July 31,2018 ili washtakiwa wasomewe maelezo ya awali (Ph). 

Katika kesi hiyo Mbowe hakuwepo mahakamani hapo na mdhamini wake aliiambia mahakama kuwa alipata taarifa Saa 10 alfajiri kuwa ameharibikiwa na gari akitokea Arusha. 

Kwa upande wa mshtakiwa wa sita ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji naye hakuwepo mahakamani ambapo mdhamini wake ameeleza kuwa amekwenda katika kesi nyingine inayomkabili huko Songea. 

Washtakiwa waliokuwepo mahakamani ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba John Mnyika, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na mbunge wa bunda, Esther Bulaya. 

Wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko. 

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam. 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad