Watu mashuhuri walio na wafuasi wengi sana kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter wamepoteza mamilioni ya wafuasi baada ya kampuni hiyo kuanza kuondoa 'watu bandia'.
Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama ni miongoni mwa walioathirika, ambapo amepoteza watu 2.1 milioni.
Bw Obama, ambaye babake alitokea Kenya, amepangiwa kuzuru tena taifa hilo la Afrika Mashariki Jumatatu 16 Julai, ziara yake ya kwanza tangu andoke madarakani.
Mwanamuziki nyota kutoka Marekani Katy Perry, ambaye ndiye mtu anayefuatwa zaidi kwenye Twitter, na Lady Gaga wamepoteza takriban wafuasi 2.5 milioni kila mmoja.
Twitter imesema imechukua hatua hiyo kutokana na juhudi zake ambazo zimekuwa zikiendelea za kujenga imani miongoni mwa wanaotumia mtandao huo.
Hii imetokea huku mitandao ya kijamii ikiendelea kuangaziwa kutokana na kueneza kwa taarifa za uzushi na watumizi feki wa mitandao ya kijamii.
Hatua mpya zilizochukuliwa na Twitter zinaathiri akaunt za Twitter ambazo zimefungwa kutokana na kutokea kwa shughuli zisizo za kawaida kwenye akaunti hizo.
Mfano wa shughuli hizi ni kufungiwa na watu, au kutuma ujumbe kwa wingi wakati mmoja mtandaoni. Aidha, kuna akaunti za watu ambao hawakujibu walipotumiwa ujumbe wa kuthibitisha utambulisho wao.
Akaunti hizi zote zinaondolewa kutoka kwenye hesabu ya watu wanaofuata akaunti mbalimbali.
Hili limeathiri watu kote duniani. Nchini Kenya, baadhi wamekuwa wakieleza idadi ya wafuasi waliowapoteza, ingawa kwa wengine idadi inashangaza.