INAUMA sana! Ndiyo maneno unayoweza kutamka baada ya mtoto wa msanii wa filamu za Kibongo, Rose Alphonce ‘Muna’ anayejulikana kwa jina la Patrick (8) ambaye alikuwa maarufu sana mitandaoni na amecheza kwenye filamu kadhaa za wasanii mbalimbali kufariki dunia ambapo kilichomuua kimebainika, Risasi Mchanganyiko linakupa habari kamili.
Mtoto huyo alifariki Jumanne jioni akiwa kwenye matibabu Nairobi nchini Kenya na kusababisha vilio kila kona; kwa wasanii hata kwa watu wa kawaida.
KILICHOMUUA NI HIKI
Akizungumza kwa njia ya simu ya mkononi kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp kabla mwanaye hajafariki Muna alisema alikuwa akisumbuliwa na uvimbe kwenye ubongo. “Kinachomsumbua mwanangu ni uvimbe kwenye ubongo na hajaamka kwa siku sita huku akiwa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalum ‘ICU’ hivyo tunasubiri aamke ndipo madaktari waangalie kama watamfanyia operesheni au la,” alisema Muna jana asubuhi na mwanaye huyo kufariki jioni.
MAMA’KE AZIMIA
Chanzo makini kilichopo Nairobi kilieleza kuwa mara baada ya mwanaye kufariki dunia, Muna alizimia kwa muda wa nusu saa kutokana na mshtuko huku anayedaiwa kuwa ni mchumba wake ambaye ni mwimbaji wa nyimbo za Injili, Joel Lwaga naye akiishiwa nguvu.
DAKTARI AANIKA CHANZO CHA UVIMBE
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, Dk Chale alisema uvimbe kwenye ubongo kitaalamu huitwa ‘Brain Tumour’ ambao unaweza kuwa wa kawaida au kansa na husababishwa na njia kuu mbili; moja ni ubongo wenyewe na pili kutokana na viungo vingine.
Katika njia ya kwanza ni kwamba inawezekana ugonjwa huu ukarithi kutoka kwa familia kama baba au mama amewahi kuwa na matatizo hayo basi lazima na wengine warithi. Sababu nyinginezo ambazo zinachangia ni maambukizi ya virusi wa ugonjwa huo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, sababu za kimazingira ambayo mtu anaishi, kemikali za viwandani, vipodozi, chakula, dawa na nyingine nyingi.
Katika njia ya pili ya viungo vingine hutokana na kama mtu ana kansa ya mapafu, kizazi, matiti, figo, tezi dume hizi huweza kusa babisha uvimbe kwenye ubongo. Dk Chale aliendelea kufafanua kuwa uvimbe kwenye ubongo kwa upande wa watoto mara nyingi huwa ni kansa na siyo wa kawaida ndiyo maana huua haraka sana na hawawezi kupona maana uvimbe huwa chini ya ubongo na siyo kwa juu kama inavyokuwa kwa watu wazima.
TUJIKUMBUSHE Kabla ya kukutwa umauti, Patrick alianza kuumwa mguu ghafla hali iliyosababishwa alazwe katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) na kufanyiwa upasuaji mara tano. Baadaye, mtoto huyo alipata ahueni na kuendelea na maisha ya kila siku.
Jana (Jumanne) asubuhi mastaa mbalimbali walionekana wakimuombea mtoto huyo apone ambapo pia mtangazaji wa Wasafi TV, Zamaradi Mketema alianza kuchangisha kwani matibabu ya mtoto huyo kwa siku sita alizokaa huko ni zaidi ya milioni 22 lakini jioni ya siku hiyo mtoto huyo akaaga dunia.