Huyu Ndiye Mtu Anayevalia Nadhifu zaidi Afrika

Unamiliki suti ngapi, viatu jozi ngapi, kofia ngapi, mashati mangapi na mikanda mingapi na soksi pea ngapi? Ukihesabu bila shaka hautakosa kugundua kuwa ni mavazi ya kukuwezesha kusukuma wiki moja au mbili hivi bila kurudia.

Lakini kwa mwanamume mmoja mwenye makao yake jijini Nairobi, Kenya hilo si tatizo.

Ana mavazi mengi ajabu, yanayojumlisha suti kamili za rangi tofauti, viatu, kofia, mikanda, saa, pete na hata mifuko ya simu, mavazi ambayo anaweza kuyavaa kwa zaidi ya siku mia moja bila kurudia.

Kila ukikutana naye kwenye mkusanyiko wa watu, hutakosa kumtambua kutokana na mtindo wake wa kipekee wa kuvalia.

Mwavuli pia nao lazima ufuate mtindo wake
James Maina Mwangi ni mzaliwa wa Muranga kati kati mwa Kenya anasema aliondoka nyumbani kwao na kuelekelea jijini Nairobi kutafuta riziki akiwa na umri wa miaka 12 baada ya kusoma hadi darasa la sita.

Anasema alipata changamoto kubwa za kuweza kupata mavazi ya kutosheleza haja yake, hasa utotoni.

"Nikiwa mdogo nilikuwa na shati moja tu nililokuwa nikilivua likikauka ninalivaa tena, na kuna wakati nilikuwa nikiazima nguo kutoka kwa marafiki kama ninataka kwenda kutembea mahali, nikimuomba rafiki ananijibu vibaya labda ananitusi au ananicheka," anasema.

"Ndipo nikamuomba Mungu anipe taji ambayo watu wengine hawana, ndio wajue kuna Mungu tofauti na yule walikuwa wanamjua," anasema Mwangi



Mwangi anasema suti moja inaweza kumgharimu kati ya shilingi 10,000 pesa za Kenya au dola 100 na shilingi 80,000 au dola 800.

Hadi sasa Bw Mwangi anasema anamiliki zaidi ya suti 150, zaidi ya jozi 200 za viatu na kofia zaidi ya 300 mavazi ambayo amekuwa akiyanunua nchini Kenya na kuagiza mengine kutoka nchini za kigeni zikiwemo Afrika Kusini, Italia, Uhispania, Ufaransa na Ujerumani.

Anasema anamiliki suti za kila rangi inayopatikana duniani na huwa kawaida anavaa rangi moja kuanzia kofia, miwani, shati, tai, suti yenyewe, viatu ,soksi saa, rangi ya simu na hata nguo za ndani.

"Mimi ni kama kioo kwa wananchi, watu wakiniona nimevaa hivi hufurahi sana, wao hunisimamisha, hunisalimia na kuzungumza nami na kunipa moyo kuendelea kuvaa hivi, na pia kuniombea mema, nafikiri ni mimi ndiye mtu maridadi zaidi Afrika," Bw Mwangi anasema.

Anasema kuwa kuvaa nadhifu lilikuwa ni ombi alilomuomba Mungu tangu utotoni na anasema kuwa atazidi kuvalia hivyo hadi ile miaka Mungu atamruhusu kuishi ulimwengu huu.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad