Idadi ya Vijana Waliookolewa Kutoka Pangoni Yafikia Nane


Idadi ya Vijana Waliookolewa Kutoka Pangoni Yafikia Nane
Shughuli ya kuwaokoa vijana 12 wa timu ya soka na kocha wao waliokwama kwenye pango kwa zaidi wa wiki mbili imechukuliwa kama mchezo wa sinema.

Ilihitajii ujasiri na weledi kutokana na mazingira magumu ya tukio hilo. Timu ya waokoaji ililazimika kunoa bongo na kuweka michoro kufanikisha kazi ya uokoaji bila ya kuathiri maisha yao na ya vijana wenyewe.

Ugumu wa kazi hiyo uliongezeka zaidi baada ya mwogeleaji mmoja kuzama maji na kufariki dunia wakati akirejea toka walikonasa vijana hao.

Uokoaji huo ambao pia unawahusisha waogeleaji wa kimataifa umefanywa kwa tahadhari kubwa hasa wakati huu ambapo mamlaka ya hali ya hewa ikionywa uwezekano wa kutokea mvua na kutatiza kazi ya uokoaji.

Tayari zaidi ya nusu ya vijana hao wameokolewa, wanne wa kwanza waliokolewa Jumapili asubuhi na baadaye kijana mwingine kuokolewa jana kabla ya idadi yao kuongezeka tena jana hiyo hiyo jioni kwa watu kuokolewa na kufikia wanane na hivyo hadi sasa pangoni wamebaki watu watano.

Maofisa wanaosimamia kazi hiyo wameanza kutoka taarifa zenye matarajio chanya kuhusiana na shughuli hiyo ya uokozi ambayo kwa kipindi kirefu imekabiliwa na vikwazo, ambavyo ni pamoja na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko.

Mapema jana kamanda wa kikosi cha uokozi, Narongsak Osottanakorn alisema awamu ya pili ya uokozi ilishaanza na kuna matarajio makubwa ya vijana hao kuokolewa wakiwa salama.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Julie Bishop ameelezea kuridhishwa na hatua iliyofikiwa hadi sasa hususan baada ya vijana hao kuokolewa.

Australia imetuma wataalamu 19, ikiwa ni pamoja na daktari ambaye amekuwa akijihusisha zaidi na kuwapima wavulana hao, na kutoa kibali cha kuwaondoa kwa kuzingatia hali yao kiafya.

Vijana hao waliookolewa wanapatiwa matibabu na familia zao bado hazijaanza kuwaona, hadi baada ya kuruhusiwa na madaktari

Ingawa walikuwa na afya njema, lakini walikuwa na njaa kali. Maofisa wamesema, vijana hao hata hivyo, wametengwa na wazazi wao kwa sasa ili kuepusha hatari ya magonjwa ya kuambukiza.

Kamanda Narungsok, amewaambia waandishi wa habari kwamba, hali ya hewa ni nzuri na kiwango cha maji ni kidogo na hivyo waliamua kuanza mapema shughuli hiyo kuliko ilivyotarajiwa.

Lakini kwa upande mwingine kamanda huyo ameelezea wasiwasi kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, baada ya mamlaka ya hali ya hewa kutangaza mvua kubwa itakayonyesha eneo hilo kuanzia jana mchana na kuendelea kwa wiki nzima, hatua inayoweza kusababisha ugumu kwenye kazi hiyo.

Operesheni hiyo ngumu ya uokozi ambayo inawashirikisha wapigambizi mahiri kutoka Thailand na nchi nyingine kadhaa za kigeni imekuwa ikifanywa kwa uangalifu mkubwa.

Kulingana na mipango ya uokozi, kila kijana alikuwa akisindikizwa na wapigambizi wawili wenye uzoefu, na walikuwa wakitolewa mmoja baada ya mwingine.

Kila kijana anavishwa kifaa maalumu cha kumsaidia kupumua ndani ya maji, huku akiongozwa kwa kamba na wapigambizi mahiri, mmoja mbele, mwingine nyuma.Baada ya kuvuka vyumba vitatu vya pango hilo, vijana hao hutembea sehemu iliyobaki ya mwendo wa takriban kilomita mbili.

Kwa ujumla wapo wapigambizi wazoefu wapatao 90 watakaohusika katika operesheni hii ya uokozi, 40 miongoni mwao wakiwa ni kutoka nchi za kigeni.

Gavana Osotthanakorn amesema baadhi ya sehemu za pango zimejaa maji hadi juu, ikimaanisha kuwa njia pekee za kuzivuka ni kupita ndani ya maji hayo ukiwa na vifaa vya hewa ya oksijeni.

Lakini kwa ujumla kiwango cha maji ndani ya pango hilo kimepungua kutokana na juhudi zilizofanywa kuyavuta nje.

Madaktari kutoka Australia waliingia katika pango hilo jana asubuhi kutathmini afya ya wavulana hao, na kutoa ripoti kwamba wanao uwezo wa kuanza safari ngumu ya kutoka nje.

Hospitali ya Chiangrai Prachunakroh iliyo umbali wa km 60 kutoka kwenye pango hilo, imejiweka tayari kuwapokea mara tu watakapofanikiwa kutoka nje.

Vijana hao waliingia katika pango hilo Juni 23 wakiwa na kocha wao mwenye umri wa miaka 25, lakini baada ya kuingia wakazingirwa na maji yaliyojazwa na mvua iliyonyesha ghafla. Wavulana hao 12 wana umri wa kati ya miaka 11 na 16. Ilichukua muda wa siku tisa kuwasaka kabla ya kugundulika kuwa walikuwa wamenasa pangoni.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad