Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP, Simon Sirro leo atafanya mabadiliko ndani ya jeshi hilo yatakayowagusa makamanda wa mikoa, wakuu wa usalama barabarani wa mikoa na wasimamizi wa usalama barabarani wa ngazi za wilaya na miji midogo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, msemaji wa jeshi hilo, Barnabas Mwakalukwa amesema uamuzi huo umefikiwa na Sirro, kwamba mabadiliko hayo yatatangazwa leo saa 10 jioni.
Amesema mabadiliko hayo yametokana na kuendelea kujitokeza kwa matukio ya ajali, yanawalenga ambao wameonyesha udhaifu katika kuzuia ajali hizo pamoja na kutodhibiti wanaokiuka sheria za usalama barabarani.
Kamanda Mwakalikwa amefafanua kuwa mabadiliko hayo yatawagusa baadhi ya makamanda wa mikoa, wakuu wa usalama barabarani wa mikoa, wasimamizi wa usalama barabarani na wa ngazi za wilaya na miji midogo.
"IGP amekemea vikali kutowajibika ipasavyo kwa baadhi ya wasimamizi wa sheria za usalama barabarani katika kudhibiti ajali jambo ambalo limekuwa likisababisha vifo na majeruhi. Ameahidi kuwa ataendelea kuchukua hatua kwa wale watakaozembea usimamizi wa sheria," Kamanda Mwakalukwa.
Aidha wasimamizi wa sheria wametakiwa kuwachukulia hatua madereva wazembe wanaoendesha kwa mwendo kasi na kutochukua tahadhari katika maeneo hatarishi barabarani.