Jeshi la Polisi yafungukia Kiini cha Ajali Mbeya


Ikiwa imepita siku 1 tangu ilipotokea ajali ya lori Jijini Mbeya katika mlima wa Igawilo na kusababisha kuua mtu mmoja, Jeshi la Polisi mkoani humo limesema limeshafahamu kiini cha ajali hizo za kila mara na kudai lina mikakati madhubuti ya kudhibiti eneo hilo kwa kushirikiana na TANROADS.


Picha hii ni miongoni mwa ajali zilizotokea katika mlima wa Igawilo siku za hivi karibuni na kusababisha kuua takribani watu watano

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, Ulrich Matei wakati akizungumza na eatv.tv leo Julai 09, 2018 na kusema eneo hilo la mlima wa Igawilo wameshafanyia uchunguzi wa kina kuhusiana na ajali zinazotokea mara kwa mara ambapo kwa sasa wamejipanga kuweka ukaguzi wa magari yote kabla hayajafika katika mlima huo pamoja na kuweka vibango vya barabara vitakavyokuwa vikitoa maelekezo husika juu ya kuwepo mlima huo ili madereva wawe makini zaidi.

"Tumeshawasiliana na  Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili kuhakikisha zile alama za barabarani zinakuwepo na hadi dakika mimi mwenyewe nipo katika huu mlima ninaona wameshafunga hizo alama za kuwajulisha madereva wote kuteremka taratibu ili wasipate ajali", amesema Kamanda Matei.

Mbali na hilo, Kamanda Matei pia ameeleza chanzo cha ajali iliyotokea usiku wa kuamkia leo katika mlima wa Igawilo na kusema lori hilo lilikuwa limebeba mbao na kusababisha kuelemewa wakati wa linataka kushuka mlima huo ndipo gari likaangukia upande mmoja huku akisisitiza kuwa ajali hiyo haijasababishwa na kugongana na gari nyingine yoyote ile.

"Ajali iliyotokea usiku wa kuamkia leo ni ajali ya kawaida tu, maana lori hilo lilikuwa limebeba mzigo wa mbao na kusababisha kulivuta gari pembeni na ndipo mzee mmoja aliyekuwepo ndani ya gari hilo kutaka kuruka ili akimbie lakini gari hilo likamuegemea", amesisitiza Kamanda Matei.

Msikilize hapa chini Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, Ulrich Matei akielezea kwa kina chanzo cha ajali hiyo pamoja na mikakati yao waliyoipanga katika kutokomeza ajali kwenye eneo hilo sugu katika mkoa huo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad