Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Phaustine Martin Kasike amefanya mabadiliko madogo ya kiuongozi kwa Wakuu wa Magereza wa Mikoa na Vituo vingine vya Magereza nchini, lengo likiwa ni kufanya maboresho ya kiutendaji.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Phaustine Martin Kasike.
Kupitia taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, na Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Lucas Mboje imetaja mabadiliko hayo ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma, Naibu Kamishna wa Magereza(DCP), Julius Sang’udi amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza kuwa Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Wafungwa na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza(SACP), Salum Hussein.
Aliyekuwa Mkuu wa Gereza Mtego wa Simba, Kamishna Msaidizi wa Magereza(ACP), Msepwa Omary amehamishiwa Magereza Mkoa wa Singida kuwa Kaimu Mkuu wa Magereza mkoa huo na nafasi yake inakaimiwa na Mrakibu wa Magereza, Muta Tibalinda.
“Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, Naibu Kamishna wa Magereza (DCP), John Masunga amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza kuwa Mkuu wa Kitengo cha Viwanda vya Jeshi la Magereza, na nafasi yake imekaimishwa kwa aliyekuwa Mnadhimu wa Magereza Mkoani Tanga, Kamishna Msaidizi wa Magereza(ACP), Emmanuel Lwinga”, imesema taarifa.
Wengine ni aliyekuwa Boharia Mkuu wa Magereza, Naibu Kamishna wa Magereza (DCP), Afwilile Mwakijungu amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza kuwa Mdhibiti Mkuu wa Shirika la Magereza na nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Magereza(ACP), Goleha Masunzu.
Jenerali Kasike anafanya mabadiliko hayo katika Jeshi la Magereza ikiwa ni wiki mbili baada ya kuteuliwa na Rais Dkt. John Magufuli kuwa Kamishna Jenerali wa jeshi hilo, akichukua nafasi ya Dkt. Juma Ali Malewa ambaye amestaafu.