JWTZ Yawatoa Hofu Wananchi Baada ya Magari yao ya Kijeshi Kuonekana Yakizunguka Ukuta wa Madini ya Tanzanite

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limefafanua sababu za kuonekana magari ya dereya eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite, Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Msemaji wa JWTZ, Kanali Ramadhani Dogoli aliliambia gazeti la Mwananchi jana kuwa magari hayo yalikuwa yakitengeneza njia kwa ajili ya doria kuzunguka ukuta uliojengwa katika eneo la migodi ya machimbo hayo.

“Hakuna operesheni inayofanyika kama inavyodhaniwa na watu, tunachokifanya ni kutengeneza njia kuzunguka mgodi ili iwe rahisi kufanya doria,” alisema.

Kanali Dogoli alisema vinavyoonekana si vifaru vya kivita, bali ni magari maalumu ya doria za kijeshi na hasa porini.

“Jeshi haliwezi kupeleka vifaru maeneo yenye makazi ya watu, vifaru vinatumika kwenye vita pekee, yaliyoonekana kitaalamu tunayaita magari ya deraya,” alisema msemaji huyo.

Kanali Dogoli aliongeza kuwa, “ukuta ule ni mrefu na hatuwezi kufanya doria kwa miguu, hivyo ni lazima tutatumia magari ambayo ni maalumu kwa njia za porini, si vifaru vile.”

Kuonekana kwa magari hayo kulizua taharuki baadhi ya wananchi wakisema ni vifaru.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula aliwatoa hofu wakazi wa Mirerani baada ya kuonekana magari hayo kuwa wao ni raia wema, hivyo hawapaswi kuogopa.

Alisema wanajeshi kazi yao ni kulinda nchi na wanatambua namna ya kulinda, hivyo hawapangiwi.

Chaula alisema wanaimarisha ulinzi nje ya ukuta na pia kuweka mazingira safi ili mtu yeyote akipita aonekane. Aliongeza kuwa, kila baada ya mita 100 kutakuwa na kibanda cha mlinzi atakayelinda ndani na nje ya ukuta.

Alisema ulinzi unaimarishwa kwa kuwa wananchi wengi wanafanya mambo kwa mazoea badala ya kufuata sheria, kanuni na utaratibu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad