MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Meddie Kagere, raia wa Rwanda, ameweka bayana kuwa malengo yake ya kwanza ndani ya timu hiyo ni kutaka kupambana kuona wanatwaa taji la Kagame Cup ambapo hadi sasa, kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Masoud Djuma, kipo hatua ya robo fainali ambayo walicheza jana Jumapili.
Kagere aliyejiunga na Simba hivi karibuni akitokea Gor Mahia ya Kenya, tayari ameonyesha makeke yake baada ya kufunga mabao mawili kwenye michuano hiyo ya Kagame Cup. Mabao hayo aliyafunga dhidi ya APR na Singida United. Jana Jumapili Simba ilikuwa na kibarua cha kuvaana na AS Port ya Djibouti katika pambano la robo fainali lililopigwa saa 1 usiku katika Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Mshambuliaji huyo ambaye alijenga pacha ya hatari na Jacques Tuyisenge wakati akiwa Gor Mahia ameliambia Championi Jumatatu, kuwa anajipanga kikamilifu katika kila mchezo ambao anashuka uwanjani kujitoa na kuipambania timu hiyo ipate ushindi kwa ajili ya kufikia malengo yake ya kutwaa ubingwa wa kombe hilo.
“Kwangu huu ni mtihani wa kwanza ambao ninatakiwa kufanikisha ninautatua, najua mashabiki wao wana kiu ya kuona kwamba tunachukua ubingwa lakini sisi tunasema kwamba tutaendelea kupambana kwa nguvu kwenye kila mchezo ambao tutashuka uwanjani.
“Mimi kwangu nitajitoa kwa kufunga kila nitakapopata nafasi ya kufunga uwanjani, hapa ndipo sehemu yangu ya kazi hivyo ni lazima nijitoe kwa kiasi kikubwa kufanikisha kila ambacho tutakuwa tunagombania ukiwemo ubingwa huu ambao upo mbele yetu,” alisema mshambuliaji huyo.