Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, ameagiza kushushwa vyeo Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Mbeya, Leopold Fungu kwa ajali zilizokithiri mkoani humo, na Mkuu wa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoa wa Kagera George Mrutu kwa kushindwa kutimiza majukumu yake.
Kangi ametoa agizo hilo leo, wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam ikiwa ni siku moja tangu kuvunja kwa Baraza la Usalama wa Barabarani Taifa hadi kwenye ngazi ya mikoa na wilaya.
“Katibu Mkuu nakuagiza kumshusha cheo Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya Leopold Fungu, kutokana na kukithiri kwa ajali za barabarani mkoani humo, na huyu Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto Mkoa wa Kagera, George Mrutu ashushwe cheo kwa matamshi yake ya sababu za yeye kutofika kuzima moto bweni la chuo”, amesema Waziri.
Katika mkutano huo Waziri Lugola, amemfukuza kikaoni Kamishna Mkuu wa Magereza, Juma Malewa kwa kuchelewa kufika kikaoni, na kuwaagiza wakuu wa idara zote za ulinzi na usalama kuja na ilani ya chama cha mapinduzi kabla ya kufanyika kwa kikao kijacho kwani wanatakiwa kufanya kazi kwa kuifuata ilani ya chama chao.