Kangi Amtwisha IGP Sirro Mzigo wa Lugumi

Kangi amtwisha IGP Sirro mzigo wa Lugumi
Mapema leo katika mkutano wake na waandishi wa habari Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro amtafute mmiliki wa kampuni ya Lugumi popote pale alipo na kumfikisha ofisini kwake Julai 31 saa mbili asubuhi ili ajue hatma yake.

Sakata la Lugumi liliibuka bungeni kwa kile kilichodaiwa kuwa zipo dalili za ufisadi, kutokana na Sh. bilioni 34 zilizolipwa kwa kampuni ya Lugumi iliyopewa tenda ya kufunga vifaa vya kielektroniki vya kutambua alama za vidole kwenye vituo vya polisi nchini.

Mradi huo uliokuwa na thamani ya Sh. bilioni 37 ambapo Mpango huo ulisukwa baada ya Bunge kupitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka 2011/12, ambayo ndani yake ilikuwa na kipengele cha ununuzi wa vifaa maalum (specialized equipment).

Mkataba huo uliingiwa mwaka 2011 baina ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi ambayo ilikuwa ifunge mashine za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo vya polisi 108 kwa gharama ya Sh. bilioni 37, hata hivyo inaelezwa ni vituo 14 tu ndivyo vina mashine hizo mpaka sasa, wakati kampuni hiyo ililipwa Sh. bilioni 34 sawa na asilimia 99 ya fedha zote kinyume cha kanuni za manunuzi ya umma, hali iliyoishtua PAC katika mkutano wake Aprili 5, 2016  jijini Dar es Salaam.


Mbali na hilo Waziri Lugola pia amemuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) afike ofisini kwake Julai 25 akiwa na waliopewa tenda ya kuleta mtambo wa kutengeneza vitambulisho vya taifa ili kwenda kumueleza kwani mtambo huo haujaletwa au waende na pesa walizopewa na Serikali.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad